CCM yadai kuna njama za vurugu Kinondoni

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kina taarifa za kuletwa kwa watu kutoka maeneo mbalimbali wakihifadhiwa katika baadhi ya nyumba katika Jimbo la Kinondoni jijini Dar es Salaam, ambao wanasingiziwa kuwa ndio wenye kulinda kura. Uchaguzi huo mdogo unaotarajiwa kufanyika kesho.

CCM imesema, imehujumiwa katika kampeni kwa kupigwa kwa vijana wao mara kadhaa katika jimbo hilo na kuwataka wananchi kuhakikisha uchaguzi huo, unakuwa wa amani, uhuru na utulivu mkubwa.

Hata hivyo, alisema hadi kufikia sasa chama hicho kiko vizuri.

Alitoa rai kwa vyama vya upinzani kuwa na uvumilivu, kwa sababu ni kawaida yao kushindwa kutokana na kupinga kila jambo, ambalo limekuwa likifanywa la maendeleo na kwamba watambue wapo wabunge makumi kwa makumi wanaoomba kujiunga na CCM kwa kuwa wananchi wanaowaongoza hawawaelewi.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema hayo jana wakati akizungumza masuala mbalimbali kuhusu uchaguzi wa mdogo kwa majimbo mawili ya Siha mkoani Kilimanjaro na Kinondoni jijini Dar es Salaam na uchaguzi wa madiwani kwa kata 10.

Kuhusu kuletwa kwa watu mikoani, alisema wapo watu wameanza kuwaondoa watu katika kushiriki katika uchaguzi huo kwa uhuru, amani na utulivu, kwa kuwa chama kina taarifa za kuletwa kwa watu kutoka mikoani kwa kisingizio cha kulinda kura ambapo wamelijulisha jeshi la polisi juu ya nyumba hizo.

“Kifuatacho ni utaalam wa kushughulika na wasioataka kufuata kanuni na taratibu za uchaguzi, kwani kura hazilindwi na watu hivihivi, upo utaratibu, mpangohuo unaweza kuwatisha wananachi kupiga kura,” alisema Polepole na kuongeza kuwa wamelieleza jeshi hilo ili watu wasiohusika kuwepo wachukuliwe hatua.

Kuhusu ushindi katika uchaguzi huo, Polepole alisema ni kawaida kwa chama hicho kushinda, na kwamba jimbo la Kinondoni lina wanachama zaidi ya 130,000 wa CCM kati ya wapiga kura 260,000 ambao kwa idadi hiyo inatosha kabisa kuonesha mtaji wa ushindi.

Alisema chama hicho hakipo kwa bahati mbaya na hawahusiki na siasa za maji taka bali wamekuwa wakijikita katika kufanya masuala ya wakati huo kwa kuhangaika na matatizo ya wananchi.