Mnadhimu Mkuu mpya aahidi kuimarisha JWTZ

MNADHIMU Mkuu mpya wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Yakubu Mohamed ameahidi kuanza na kazi ya kuliimarisha jeshi hilo.

Yakubu aliitoa hadi hiyo jana baada ya kuapishwa na Amiri Jeshi Mkuu, Rais John Magufuli, Ikulu jijini Dar es Salaam kushika wadhifa huo.

Mbali ya kumshukuru Rais Magufuli kwa kumuamini na kumpa nafasi hiyo, alisema atatekeleza mara moja agizo la kuliimarisha zaidi jeshi hilo kuzidi lilivyo sasa.

"Kazi yangu pamoja na wenzangu wapya ambao wamepandishwa vyeo ni kutengeneza mikakati ya kutekeleza ahadi ya CDF (Mkuu wa Majeshi) ya kuhakikisha tunaliimarisha zaidi jeshi," alisema Luteni Jenerali Yakubu.

Alisema anaamini atapata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa watendaji wenzake. Luteni Jenerali Mohamed amechukua nafasi ya Luteni Jenerali James Mwakibolwa ambaye amestaafu hivi karibuni.

Awali, Mkuu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo aliwavisha vyeo Meja Jenerali wapya baada ya kupandishwa vyeo kutoka MaBrigedia Jenerali na Rais Magufuli juzi. Jenerali Mobeyo pia alitangaza mabadiliko ndani ya jeshi hilo baada ya maofisa wengine kustaafu.

Katika nafasi hizo mpya, Meja Jenerali Martin Busungu anakuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali George Msongole anakuwa Mkuu wa Jeshi la Nchi Kavu na Meja Jenerali Jacob Kingu anakuwa Mkuu wa Chuo cha Ulinzi wa Taifa.

Wengine ni Meja Jenerali Alfred Kapinga ambaye anakuwa Mkuu wa Mafunzo na Utendaji Kivita Jeshini, Meja Jenerali Blasius Masanja Mkuu wa Utumishi Jeshini na Meja Jenerali Anselm Bahati kuwa Mkuu wa Shirika la Nyumbu.

Wengine ni Meja Jenerali Kaisy Njelekela kuwa Jaji na Wakili Mkuu wa Jeshi, Meja Jenerali Shija Makono kuwa Mkuu wa Shirika la Mzinga Mazao, Meja Jenerali Ramadhani Mrangira kuwa Kamishna wa Maendeleo, Sera na Mipango katika Wizara ya Ulinzi na Meja Jenerali Mathew Mkingule kuwa Mdhibiti Mkuu wa Fedha Jeshini.

Mnadhimu Mkuu mstaafu wa JWTZ, Luteni Jenerali Samuel Ndomba alimuasa Meja Jenerali Yakubu, kutofanya kazi kwa kuangalia ukabila, udini wala jamaa, bali kuweka mbele maslahi ya taifa.

"Inawezekana marafiki wamesema Mungu atupe nini na sisi tumepata mtu wetu, au ndugu nao wakasema hivyo, lakini ukumbuke wewe unatumikia jeshi na si kwa manufaa yao, wewe ni wa watu wote, dini zote, makabila yote," alisema.

Alimuasa kuangalia familia isivae koti lake na alimuasa pia kufanya kazi na wakati huo huo kuangalia familia.

Meja Jenerali Mwakibolwa alimuasa Luteni Jenerali Yakubu, kubadilika kutokana na matukio ya matishio katika dunia ya sasa na kuwa mkali ndani ya jeshi.

Luteni Jenerali mstaafu, Michael Mwakalindile aliwaasa viongozi hao wapya, kufanya kazi kuendeleza ahadi waliyoitoa katika viapo vyao vya jeshi. Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi alimshukuru Rais kwa kuendelea kuwa karibu na majeshi, ambapo alisema pia kuwa sasa majeshi yako vizuri.