Meli za abiria Ziwa Victoria zakarabatiwa

JUMLA ya meli tano zitakazokuwa zinafanya kazi ya usafirishaji abiria ndani ya Ziwa Victoria zilizokuwa zikifanyiwa matengenezo na Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) zimekamilika na zitaanza kutoa huduma ya usafiri wakati wowote kuanzia sasa.

Hayo yalielezwa jana na Kaimu Meneja Mkuu wa MSCL, Erick Hamisi alipokuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma ya ukataji tiketi kwa mfumo wa kielektroniki na ukaguzi wa Meli ya Mv Clarias baada ya kufanyiwa ukarabati.

Alizitaja meli hizo kuwa ni Mv Clarias, meli ya mizigo Marine Lighter (Wimbi), Mv Umoja, Marine Takner (MT) Sangara na Mv Liemba. Kati ya meli hizo, meli tatu yaani meli ya mafuta ya Marine Tanker - MT Sangara iliyoko mkoani Kigoma, meli ya mizigo ya ML Wimbi na Mv Clarias zilizoko jijini Mwanza zimekarabatiwa kwa kutumia mkopo usiokuwa na riba na wenye masharti nafuu wa Sh milioni 300 kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA).

Alisema ujenzi wa meli hizo tano ni sehemu ya mkakati wa muda mfupi uliobuniwa na Menejimenti ya MSCL ulioanza mwezi Januari, mwaka jana na kumalizika mwezi Desemba, mwaka huu kwa ajili ya kurejesha na kuboresha huduma zake za kusafirisha kwa usalama abiria na mizigo ambao uliidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi ya MSCL.

Alisema kwa upande wa meli ya MV Clarias ambayo jana ilikaguliwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa na ambayo ukarabati wake ulianza mwezi Julai, mwaka jana na kukamilika mwezi Desemba, mwaka huo kwa gharama ya Sh milioni 132.8 ina uwezo wa kubeba abiria 300 na tani 10 za mizigo.

Alisema ukarabati wa meli hiyo ulihusisha marekebisho ya injini zote mbili, ukarabati wa gia boksi, uvungu wa meli, uundwaji wa viti vya abiria, utengenezaji na uwekaji wa madirisha ya vyoo, ukarabati wa mifumo ya mabomba na umeme na ukarabati wa vyoo.

Katika hatua nyingine, Hamis alimshukuru Rais John Magufuli kwa kutekeleza ahadi zake za uchaguzi, ambapo aliahidi ujenzi wa meli kubwa ya kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Victoria.

Alisema tayari serikali imeshatenga fedha na kuipatia MSCL sehemu ya fedha ya ujenzi wa meli hiyo na kwamba taratibu za kukamilisha makubaliano na Mkandarasi wa meli hiyo aliyeteuliwa zinaendelea.

Alisema mwezi ujao MSCL itatangaza rasmi ujenzi wa meli mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 200 za mizigo katika Ziwa Tanganyika ambapo meli zote hizo zitamilikiwa na kuendeshwa na MSCL. Profesa Mbarawa alisema atafuatilia kwa karibu ili kuhakikisha kuwa ujenzi wa meli hiyo mpya unakamilika kwa wakati uliopangwa.