Musyoka: Siondoki NASA

NAIBU Kiongozi wa Muungano wa vyama vya upinzani nchini Kenya (Nasa), Kalonzo Musyoka amesema yupo tayari kumuunga mkono kiongozi wa muungano huo, Raila Odinga, lakini hataki kuapishwa kuwa Naibu Rais. Mwanasiasa huyo alikuwa mgombea mwenza wakati wa uchaguzi wa Rais uliofanyika Agosit nane mwaka jana.

Musyoka amekanusha taarifa zinazodai kuwa anajiandaa kuapishwa kuwa Naibu Rais wa Wananchi wa Kenya, Februari 28, mwaka huu.

Kalonzo ametoa msimamo huo wakati anazungumza na katika mkutano wa wanawake, na amekanusha tuhuma zinazodai kuwa yeye na viongozi wenzake wawili wa Nasa wana mpango wa kuanzisha muungano mwingine bila kumshirikisha Odinga.

Mmoja wa waliokuwa wakimuunga mkono Musyoka amesema katika kipindi cha mahojiano cha televisheni kuwa mwanasiasa huyo, Musalia Madavadi wa chama cha ANC na Moses Wetangula wa Ford Kenya wanatengeneza muungano mpya kwa ajili ya kujiandaa na Uchaguzi mkuu wa Mwaka 2022.

Naibu huyo alisema bado anapenda kuendeleza ushirikiano wake na Odinga na ataendelea kumuunga katika kusajili rasmi muungano huo wa Nasa.

“Nilisimama na Odinga mwaka 2013, nikasimama naye tena mwaka jana na nitasimama tena kama nitahitajika. Mimi si kiongozi mbinafsi. Odinga na mimi ni kama mapacha na mtu yeyote anayefikiria kuivuruga Nasa, ajaribu kufikiria tena,” amesisitiza Musyoka.

Amesisitiza kuwa hajawahi kufikiria kuicha NASA.

“Nipo hapa na sitaondoka. Tulikuwa na tatizo na NRM, lakini tayari ufumbuzi umepatikana,” amesema.

Amemuonya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) wa Kenya, Joseph Boinnet na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, Githu Muigai, kwa kumdharau endapo hawatompatia taarifa za usalama wake ndani ya siku tatu.