Makonda apokea makontena 20 yenye samani

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameahidi kuwajengea walimu nyumba ili kutatua changamoto zinazowakabili yakiwemo makazi.

Ametoa ahadi hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati anapokea makontena ya samani zitakazotumika katika ofisi za walimu zinazoendelea kujengwa.

Msaada huo wa makontena 20 ya samani za maofisini zenye thamani ya shillingi bilioni 2 umetolewa na Watanzania wanaoishi Marekani wanaojulikana kama Six Region Diaspora Council.

"Walimu wangu wengi kuna ambao washachukua viwanja. Wapo watu wanadesign aina tofauti tofauti za nyumba halafu hizo ramani tutazileta kwenu kupitia afisa elimu na gharama zake tushaagiza ziwe ndogo kadri inavyowezekana.

"Mwaka jana wakati nimetembelea China, kuna nyumba zimejengwa bila kutumia saruji lakini zina uwezo wa kudumu miaka 80. Wameahidi watakuja kutujengea nyumba za mfano. Watajenga mfano wa nyumba chache kwa maafisa elimu. Lengo ni kuona walimu wanatoka kwenye nyumba nzuri, wanafanya kazi kwenye ofisi nzuri ili tuwe na matokeo mazuri," amesema Makonda.