Dk Mndolwa Askofu Mkuu mpya Anglikana

KANISA la Anglikana Tanzania limemchagua Askofu Dk Maimbo Mndolwa (49) kuwa Askofu Mkuu wake wa Saba. Askofu Mndolwa amechukua nafasi ya Askofu Dk Jacob Chimeledya, ambaye amemaliza muda wake.

Askofu mpya atatumikia cheo hicho kwa miaka mitano. Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu uchaguzi huo, Katibu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk Mecka Ogunde alisema sinodi maalumu ya uchaguzi, imefanyika kwa mujibu wa Katiba ya kanisa hilo.

"Askofu huyu ni Askofu wa Dayosisi ya Tanga na alipewa daraja la uaskofu na kuwekwa wakfu Septemba 4, mwaka huu," alisema Dk Ogunde.

Alibainisha kuwa Askofu huyo mteule, aliyechaguliwa juzi, atasimikwa rasmi kuanza kushika wadhifa huo Mei 20, mwaka huu Siku ya Pentekoste katika Kanisa la Anglikana Dodoma.

Katibu huyo alisema Askofu Mndolwa, aliwaeleza wajumbe na umma kwa ujumla amepokea kwa unyenyekevu nafasi hiyo na kuahidi kufanya kazi kwa manufaa ya umma na kanisa.

Alisema Askofu huyo alisisitiza amani, mshikamano na kumsikiliza Mungu katika maisha yake. Mwanasheria wa kanisa hilo, George Mandepo alisema Askofu huyo amepatikana kwa kupigiwa kura na maaskofu wote.

“Tuna dayosisi 28 zilizokuwepo ni 25 ambapo wote wamethibitisha kumchagua Askofu Mndolwa. Hawa wote 25 waliingizwa kwa awamu ya kwanza na mchakato huu unapigiwa kura mara tatu hadi anapatikana," alisema.