CWT yamchongea mkuu wa shule kwa mkurugenzi

CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT), Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa kimemtaka Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Missana Kwangula kumvua madaraka Mkuu wa Shule ya Sekondari Kabwe, Jackson Mussa kwa kuwa amepoteza sifa za uongozi.

Katibu wa CWT Wilaya ya Nkasi, Herry Mtovano akizungumza na gazeti hili alisema chama hicho kinalaani kitendo cha Mussa kumdhalilisha mwalimu mwenzake, Emmanuel Mbemba kwa kumpiga ngumi na vibao mbele ya wanafunzi wake.

Mtovano alidai licha ya Mussa kumpiga ngumi na makofi mwalimu mwenzake Mbemba pia alimtoa ofisini kwake, akimsukuma kwa nguvu tukio lililoshuhudiwa na wanafunzi na jumuiya ya shule hiyo.

Alisema walituma shuleni hapo timu iliyoongozwa na Ofisa Elimu Kata ya Kabwe, Geoffrey Mtafya na Kiongozi wa CWT Mahali pa Kazi, Eliya Eliya ambaye pia ni mwalimu shuleni hapo, ambao wamethibitisha tukio hilo.

"Mkuu wa Shule (Mussa) amepoteza sifa ya uongozi badala ya kutumia sheria ametumia nguvu kubwa kushambulia mwalimu wake (Mbemba), hivyo tunamuomba Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya atengue madaraka yake na amchukulie hatua nyingine za kinidhamu,” alisisitiza kiongozi huyo wa CWT.

Alisema asubuhi ya Alhamisi iliyopita, Mbemba ambaye anafundisha somo la jiografia Kidato cha Nne, alimuomba mkuu wake wa shule (Mussa) amwandikie barua ya ruhusa ili aende na wanafunzi wa darasa hilo katika ziara ya mafunzo katika fukwe za Ziwa Tanganyika. Shule ya Sekondari ya Kabwe iko mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi.

"Mussa alikataa kuandika barua hiyo akidai kuwa kuna ukaguzi wa ndani ndipo walipoanza kubishana .... alighadhabika, akamkwida Mbemba na kuanza kumpiga makofi huku akimsukuma atoke nje ya ofisi kisha akaendelea kumpiga ngumi mbele ya wanafunzi wake,” alidai Mtovano.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Kwangula alikiri kutokea kwa tukio hilo ila alisisitiza baadaye hatua zitachukuliwa dhidi yake baada ya kupokea taarifa kamili.

Aidha, mkuu huyo wa shule amekanusha kumpiga makofi, ngumi Mbemba isipokuwa alimkwida shingoni.