Ujenzi daraja la Mto Mara kukamilika Aprili

SERIKALI imesema ujenzi wa daraja la Mto Mara lenye urefu wa mita 94 lililopo katika Barabara ya Tarime-Mugumu-Nata linalounganisha wilaya ya Tarime na Serengeti, litakamilika mwanzoni mwa Aprili mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini cha Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, kukamilika kwa mradi huo itakuwa dira kwa makandarasi wazawa kupewa miradi mikubwa kwani pamekuwa na changamoto kwenye utekelezaji wa miradi hususani kwa makandarasi wazawa.

Taarifa hiyo ilieleza kwamba Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akikagua ujenzi wa daraja hilo aliwatoa hofu wananchi wa wilaya hizo na kusema endapo daraja hilo litakamilika litaondoa adha waliyokuwa wanaipata ya kuvuka hasa vipindi vya masika.

“Niwahakikishieni daraja hili litamalizika mapema mwezi wa nne pia nimemuagiza mkandarasi huyu ambaye ni mzawa kuhakikisha anazingatia viwango na wakati,” alisema Profesa Mbarawa.

Mkandarasi wa Kampuni ya M/S Gemen Engineering & Mayanga, Andrew Nyamtori, alisema mradi huo umekamilika kwa sehemu kubwa, kazi zilizobakia ni kutandika vyuma juu ya daraja ili likamilike na kuanza kutumika.

Aliiomba serikali kuendelea kuwaamini makandarasi wazawa kwa kuwapa miradi mingine mikubwa ili waoneshe uwezo wao. “Nikuhakikishie Waziri kwamba, mradi huu utakamilika kwa viwango hivyo naomba utuamini na hata zikitokea kazi nyingine naomba tupewe kipaumbele cha kuzitekeleza kwa kuwa tunaweza,” alisema.

Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Mara, Mlima Ngaile alisema watahakikisha wanamsimamia vizuri mkandarasi ili aweze kutekeleza mradi huo kwa viwango vyote.

Katika hatua nyingine, Profesa Mbarawa amekagua Kiwanja cha Ndege cha Musoma na kueleza kuwa serikali tayari imeshatangaza zabuni ya upanuzi wa kiwanja hicho na wakati wowote zabuni zitafunguliwa ili mzabuni apatikane.