Majaliwa aonya wakulima kuchanganya pamba na mchanga

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wakulima wa pamba kutochanganya pamba na mchanga au maji kwa sababu watakosa wanunuzi.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wilayani Kwimba, kwamba serikali itapambana na watu wote wanaotaka kuvuruga zao hilo.

“Wakulima msichezee pamba kwa kuichanganya na chochote ili kuiongezea uzito kwa sababu mtaharibu sifa nzuri ya pamba ya Tanzania ndani na nje ya nchi,” alisema na kuonya tabia ya baadhi ya wakulima wanaochanganya pamba, maji au mchanga kabla ya kupeleka zao hilo sokoni wakilenga kuiongeza uzito.

Waziri Mkuu alisema serikali imeanza kuona tija tangu ilipoagiza maofisa kilimo katika mikoa inayolima pamba wasimamie kilimo hicho kuanzia ngazi za awali.

Akizungumzia suala la wanunuzi wa pamba, Waziri Mkuu alisema tayari serikali imeweka mikakati ya kutosha itakayowezesha pamba yote kununuliwa.

Kuhusu suala la bei, alisema wataangalia katika soko la dunia na kisha watawashawishi wanunuzi wanunue kwa bei nzuri itakayowanufaisha wakulima.