CCM yakomboa majimbo ya Siha, Kinondoni

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimefanikiwa kuyarejesha majimbo ya Siha mkoani Kilimanjaro na Kinondoni yaliyokuwa chini ya vyama vya upinzani.

Wagombea wa CCM wamepata ushindi katika uchaguzi mdogo uliofanyika jana.

Baada ya uchaguzi mkuu, 2015, Chadema ilishinda katika Jimbo la Siha kupitia Dk Godwin Mollel huku Cuf ikilitwaa jimbo la Kinondoni kupitia kwa Maulid Mtulia.

Wabunge hao walihama upinzani kwa kile walichokieleza kuwa wanaunga juhudi za serikali iliyopo madarakani, jambo ambalo liliifanya Tume ya Uchaguzi (Nec) kuitisha uchaguzi mdogo katika majimbo hayo mawili.

Kwa mujibu wa Nec jimboni Siha, Dk Godwin Mollel amepata ushindi kwa kupata kura 25,611, mpinzni wake, Elvis Mosi wa Chadema amepata kura 5,905.

Kwa upande wa Kinondoni, tume hiyo imemtangaza Mtulia kuwa mshindi kwa kura 30,247, akifuatiwa na Salum Mwalimu wa Chadema aliyepata 12,353, Rajab Salum wa CUF (1,943) na Ally Abdallah wa ADA-TAPEA (97).