Tanesco yadai mashirika ya serikali bil.297/-

WAZIRI wa Nishati, Dk Medard Kalemani amesema Shirika la Umeme nchini (Tanesco) linayadai mashirika ya serikali Sh bilioni 297/-.

Alisema hayo juzi kabla ya kuwasha umeme katika kijiji cha Negezi na mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Mwamashele wilayani Kishapu mkoani hapa, ambako alielezwa kero ya kukatwa umeme kwenye kituo kikuu cha usambazaji maji cha Ihelele, hali inayofanya wananchi kukosa huduma ya maji.

Dk Kalemani alisema hadi sasa mashirika ya serikali yanadaiwa na Tanesco Sh bilioni 297, hali inayoweza kushusha ufanisi wa kazi wa shirika hilo. Hivyo, alitaka mashirika hayo kulipa madeni hayo haraka.

“Naishukuru Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya Kahama na Shinyanga (Kashwasa) kwa kuanza kulipa kiasi cha Sh milioni 800 na bado Sh bilioni 1.4, mazungumzo yanaendelea ya kuona namna ya kulipa deni lote kidogo kidogo na kulipa ankara inayoendelea kutumika,” alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack alimuomba Kalemani kuwa wakati wanaendelea na mazungumzo na Kashwasa, wasikate maji ili wananchi waendelee kupata huduma ya maji.

Alisema ambazo Tanesco imezitoa kwa Kashwasa kulipia deni ni chache, ila nao wajipange kulipa madeni hayo. Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kashwasa, Lawrence Wasala alisema Tanesco ilikuwa ikiwadai Sh bilioni 2.2, lakini tayari wamelipa Sh milioni 800.

Alisema kufikia mwisho mwa mwezi huu, wanatakiwa kumalizia deni lote lililobaki la Sh bilioni 1.4; na wameelezwa kuwa wasipofanya hivyo, watakatiwa tena umeme.