Aliyempa Grace Mugabe PhD akamatwa

WACHUNGUZI wa rushwa nchini Zimbabwe wamesema wamemkamata mhadhiri wa chuo kikuu akituhumiwa kwa ulaghai wa kumtunukia shahada feki ya udaktari wa falsafa (PhD), mke wa Rais wa zamani wa nchi hiyo, Grace Mugabe.

Levi Nyagura ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Zimbabwe, alikamatwa na Tume ya Kupambana na Rushwa ya Zimbabwe (ZACC) baada ya kufanyia uchunguzi PhD ya Grace.

Ilibainika kuwa Grace alitunukiwa shahada na chuo hicho mwaka 2014, mwezi mmoja baada ya kusoma. Kwa kawaida shahada hiyo ya juu inahitaji miaka saba kamili ya utafiti na kuandika.

"Nyagura amekamatwa. Hatuwezi kuwa na watu wanaotoa shahada feki,” alisema Kamishna wa ZACC, Goodson Nguni. Profesa huyo atashitakiwa kwa kutumia vibaya ofisi yake, alisema kamishna na kukataa kubainisha iwapo Grace pia atakamatwa.

Kiu ya Grace Mugabe kutaka kumrithi urais mumewe mwenye umri wa miaka 93 ililisukuma jeshi la Zimbabwe kuchukua mamlaka na kumng’oa Robert Mugabe madarakani Novemba, mwaka jana.

Makala ya kurasa 226 tasnifu ya udaktari yenye kichwa cha habari "The Changing Social Structure and Functions of the Family" ilichapishwa mwezi uliopita baada ya shinikizo la umma kutaka Grace anyang’anywe PhD yake.

Wakosoaji wanasema Grace (52), hakusoma au kufanya utafiti kupata udaktari huo.

Alikingiwa kifua binafsi na Rais Mugabe, ambaye wakati huo pia alikuwa Kansela wa Chuo Kikuu.