Wakenya waja kumpongeza mbunge Longido

WANASIASA kadhaa kutoka Kajiado, Kenya ni miongoni mwa wageni mbalimbali wa ndani na nje ya nchi na wananchi waliohudhuria sherehe za shukrani kwa ajili ya Mbunge mpya wa Longido, Arusha, Dk Stephen Kiruswa (CCM).

Wanasiasa hao wa Kenya ni Mbunge wa Jimbo la Kajiado Magharibi wa chama tawala cha Jubilee, George Ole Sunguyia, Gavana Joseph Ole leng J u na madiwani saba wa jimbo hilo.

Viongozi hao wakiwa na wananchi walifika Longido kumpongeza Dk Kiruswa (CCM) aliyechaguliwa mbunge mapema mwaka huu.

Sherehe ya kumpongeza iliyoandaliwa na wananchi wa Longido ilienda sambamba na zawadi alizokabidhiwa mbunge, ng'ombe, mbuzi zaidi ya 150 na mavazi ya kimila na kuombewa na wazee wa mila ya jamii ya kifugaji maarufu kwa jina la Laigwanani.

Mbunge huyo kutoka Kenya na Gavana walisema wamekuja kushiriki na wananchi wa Longido kumpongeza Dk Kiruswa kwa kuchaguliwa kuwa mbunge na kusema kuwa wananchi hawakufanya makosa kumchagua.

Mbunge Sunguyia alisema yeye na wanasiasa wenzake wanamjua vizuri mbunge huyo kwa utendaji kazi na ufuatiliaji na ni kiongozi asiyekuwa na makuu na ni kiongozi wa watu na ndio maana wamekuja kumuunga mkono.

Alisema Wakenya wote wanamheshimu Rais John Magufuli na kumwona kiongozi shupavu mwenye kufuatilia mambo muhimu ya maendeleo hivyo akiungana na mbunge Dk Kiruswa Longido itapaa kwa maendeleo.

Mbunge huyo pia alisema lengo wamekuja ili kuendeleza uhusiano mzuri wa Tanzania na Kenya ili kila mwananchi afurahie fursa zilizopo Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Mgeni rasmi katika sherehe hizo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Lootha Sanare alisema kilichosemwa na mbunge kutoka Kenya juu ya uhusiano kinapaswa kuangaliwa kwa jicho la tatu kwani ni muhimu ili kudumisha ujirani mwema na kusisitiza kuwa ni lazima sheria za nchi zote wanachama ziheshimiwe pia.

Dk Kiruswa alisema atatekeleza vipaumbele alivyoahidi wakati akiomba kura na kujenga uhusiano mzuri na wananchi wa Longido.