EAC yaungwa mkono kuacha mitumba

WAKATI Marekani ikitishia kuziwekea vikwazo nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) endapo zitaanza kutekeleza uamuzi wake wa kuachana rasmi na nguo za mitumba, wakuu wa nchi hizo wametakiwa kutorudi nyuma.

Wakuu wa nchi za EAC ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini, Machi mwaka 2016 walipitisha azimio la nchi wanachama kuachana rasmi na uagizaji wa nguo za mitumba ifikapo mwaka kesho, lengo likiwa ni kulinda viwanda vya ndani.

Ukiwa umebaki mwaka mmoja kabla ya kuanza kwa azimio la kutoingiza mitumba katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Marekani kupitia kwa Kaimu Mkuu wa Idara ya Uchumi na Ushirikiano wa Kikanda barani Afrika, Harry Sullivan imedai kuwa, Rwanda, Tanzania na Uganda zinapaswa kufikiria upya uamuzi wake, vinginevyo zinaweza kukabiliana na adhabu.

Msimamo wa kutolegeza kamba katika kudhibiti mitumba, umetolewa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Biashara Afrika Mashariki (EABC), Lilian Awinja alipokuwa anazungumzia yaliyojadiliwa katika mkutano wa bodi ya baraza hilo uliofanyika hivi karibuni jijini Kigali, Rwanda.

Alisema suala la viwanda Afrika Mashariki linapaswa kuwa na msukumo wa pamoja, kwani tayari viongozi wakuu walishatoa maelezo, hasa katika kuongeza tija katika kilimo cha pamba na viwanda vya nguo.

Aliongeza kuwa, licha ya kwamba zinatarajiwa kuwepo kwa changamoto katika hatua za awali za utekelezaji, watu wasirudi nyuma, kwani kufanya hivyo kuna faida nyingi kuliko hasara.

Alitoa mfano kuwa, kushamiri kwa kilimo cha pamba na viwanda vya nguo kutachangia ukuaji wa soko la ajira katika kilimo na hata viwanda, hivyo kukuza uchumi wa nchi wanachama ambazo kwa ujumla wake una takribani watu milioni 170.

“Tunataka viwanda vyetu vianze kutumia malighafi za ndani ya jumuiya, si kutoka nje kama ilivyo sasa. Serikali zetu lazima ziwekeze sana ili kupunguza gharama za uzalishaji na kusaidia biashara zaidi ndani ya ukanda wetu,” alisema.

Aliongeza kuwa, katika kikao hicho EABC wamejadili mambo mengi yenye kulenga ustawi wa biashara, hasa mazingira yanayoweza kuvutia wawekezaji zaidi, huku akisema nchi zinapaswa kuamka na kuwa na ushirikiano katika kuvutia wawekezaji, badala ya kuwakatisha tamaa na kuwakimbiza.

Azimio la wakuu EAC Machi 3 mwaka 2016, viongozi wakuu wa nchi za EAC waliokutana jijini Arusha, Tanzania waliazimia kupiga marufuku uagizaji wa nguo na viatu vya mitumba, huku utekelezaji wake ukitakiwa kuanza baada ya miaka mitatu, yaani ifikapo mwaka kesho Marufuku hiyo ni moja ya hatua zilizopendekezwa ili kuinua viwanda vya nguo katika Ukanda ya Afrika Mashariki.

Serikali za Afrika Mashariki zimekuwa zikilaumu uagizaji wa nguo na viatu vilivyotumika kama moja ya sababu zinazofanya viwanda vya nguo na ngozi kusambaratika, hivyo kuwanyima wenyeji nafasi ya ajira.

Kwa sasa, nguo za mitumba zimekuwa tegemeo kwa watu wengi wa kipato cha chini, huku pia zikigeuka kuwa ajira kwa wauzaji wake, wasafirishaji na waagizaji katika maeneo mengi.

Nchini Tanzania, serikali kupitia viongozi wakuu wamekuwa wakisisitiza kwamba nchi iko mbioni kuachana na matumizi ya nguo za mitumba kwa kuwa nguo nyingi zitakuwa zinatengenezwa nchini, hivyo kupatikana kwa bei nafuu.

Katikati ya mwaka jana, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa katika ziara ya kutembelea kiwanda cha nyuzo cha Namera kilichopo Gongolamboto na kiwanda cha nguo cha Nida kilichopo Ubungo, vyote vya jijini Dar es Salaam, alisema safari ya Watanzania kuachana na nguo za mitumba imewadia kutokana na uwepo wa viwanda vya kutengeneza nguo nchini.

Pia aliwapa matumaini wakulima wa pamba na kusema hawana sababu ya kwenda kuuza nje ya nchi, badala yake wauze pamba hiyo katika viwanda vya ndani ili vizalishe nguo za kutosha zitakazouzwa nchini kwa gharama nafuu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alisema Tanzania imeazimia kuachana na biashara ya kuingiza nguo za mitumba kutoka nje kama ilivyokuwa kwa nchi wanachama wa EAC.

Akizindua uzinduzi wa mafunzo ya uanagenzi ya ushonaji nguo katika kiwanda cha Tanzania Tooku Garments Ltd kinachouza nguo zake Ulaya na Marekani, alisema wakuu wa EAC wamekubaliana ifikapo mwaka 2019 soko la Afrika Mashariki halitaingiza nguo za mitumba kutoka nje