Viwanja 800 Dodoma kuuzwa mwezi huu

MANISPAA ya Dodoma imepima viwanja 800 ambavyo inakusudia kuviuza kwa wananchi mbalimbali mwishoni mwa mwezi huu.

Akizungumza na HabariLeo, Mkurugenzi wa Manispaa, Godwin Kunambi alisema mkakati wa halmashauri ni kuhakikisha wafanyakazi na wageni wanaokuja Dodoma wanapata viwanja.

Alisema hiyo ni awamu ya kwanza, awamu ya pili inakusudia kupima viwanja zaidi ya 15,000 katika maeneo mbalimbali ikiwamo la Nala, Mtumba na Mkonze kwa ajili ya watu kununua.

Kunambi alisema halmashauri hiyo imekuwa ikijipanga kuhakikisha masuala ya viwanja kwa watu wanaokuja kufanya kazi mjini Dodoma, hivyo kuufanya upangike na watu wasikose viwanja vya kujenga.

Hivi sasa manispaa inafanya marekebisho ya baadhi ya maeneo, viwanja na misingi ambayo ilikuwa imejengwa bila utaratibu kuhakikisha wananchi wanajenga vizuri bila kuwa na makazi holela.