12,000 hawakumaliza elimu ya msingi Dodoma

JUMLA ya wanafunzi 12,054 sawa na asilimia 22.23 walioanza darasa la kwanza mwaka 2011, wameshindwa kumaliza masomo mwaka 2017 katika halmashauri zote mkoani humo.

Takwimu hizo zilitolewa na Ofisa Elimu wa Mkoa wa Dodoma, Maria Lyimo kwenye mkutano wa wadau wa elimu, ulioitishwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kujadili kuporomoka kwa ufaulu wa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika mkoa huo.

Lyimo amesema, idadi ya wanafunzi walioishia njiani imepungua kidogo kuliko ile ya wale walioanza masomo mwaka 2010 na kuhitimu mwaka 2016, ambapo wanafunzi 12,406 hawakumaliza masomo sawa na asilimia 24.95.

Lyimo alisema Wilaya ya Chamwino ndiyo iliyoongoza kwa kuwa na wanafunzi wengi zaidi ambao ni 2,085 kwa walioshindwa kuhitimu masomo mwaka 2017, wakati walioshindwa kuhitimu mwaka uliotanguliwa walikuwa wanafunzi 2,124.

"Wilaya iliyofuata kwa kuwa na wanafunzi wengi walioishia njiani ni Kongwa ambayo zaidi ya wanafunzi 2,114 walishia njiani kwa sababu mbalimbali hawakuhitimu mwaka 2017," alisema.

Katika orodha hiyo, Wilaya ya Mpwapwa ilikuwa na zaidi ya wanafunzi 1,806 ambao walianza mwaka 2011 na wakashindwa kuhitimu masomo yao mwaka 2017.

Lyimo alizitaja wilaya nyingine katika mkoa huo kuwa ni Chemba ambayo wanafunzi 1,854 hawakuhitimu masomo mwaka 2017, Bahi (1,596), Dodoma Manispaa (1,525), Kondoa Vijijini (852) na Kondoa Mjini (222).

Mkoa wa Dodoma una shule za msingi 765, kati ya hizo shule shule za serikali ni 727 na shule 38 za watu binafsi.