Mawaziri kujibu hoja za kamati za Bunge

MAWAZIRI wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wametakiwa kujitayarisha na kujibu hoja za ripoti za kamati za Baraza la Wawakilishi zilizowasilishwa na wenyeviti wake  Septemba mwaka jana.

Hayo yalisemwa na Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mgeni Hassan Juma wakati akitoa ufafanuzi katika utaratibu wa kujibu hoja za kamati za Baraza la Wawakilishi zilizowasilisha ripoti zake mbele ya wajumbe.

Juma alisema kwa mujibu wa kanuni za Baraza la Wawakilishi mara baada ya ripoti za kamati kuwasilishwa na wenyeviti wajumbe watazichangia na baadaye mawaziri husika kujibu hoja baada ya kufanya utafiti wa taarifa na michango ya wajumbe.

Alisema ili kuwawezesha mawaziri husika kujibu hoja hizo kikamilifu, kamati ya uongozi ya Baraza la Wawakilishi umewataka mawaziri kujibu hoja hizo katika kikao cha Septemba mwaka huu.

“Waheshimiwa mawaziri mnachotakiwa kwa mujibu wa kanuni za baraza ni kupokea taarifa hiyo na baadaye mnatakiwa kuifanyia kazi na kuja kutoa taarifa yake mwezi wa Septemba mwaka huu,” alisema.

Alisema yapo mambo ambayo mawaziri wanaweza kujibu hoja hizo kwa kuzitolea ufafanuzi, lakini baadhi ya taarifa zinahitaji ufafanuzi wa kina ambao utawahusisha watendaji wa wizara, ikiwemo makatibu wakuu na wasaidizi wake.

Alisema baadhi ya hoja zilizotolewa katika taarifa ya kamati pamoja na michango ya wajumbe ambazo zinahitaji taarifa ya kitaalamu ni pamoja na suala la kuharibika kwa meli ya MV Mapinduzi.

Wajumbe wengi wa baraza la wawakilishi waliitaka Serikali kutoa ufafanuzi kuhusu kuharibika kwa meli ya abiria ya Mv Mapinduzi ambayo imesitisha safari zake za kutoa huduma za abiria kati ya visiwa vya Unguja na Pemba.

Jumla ya kamati sita za baraza la wawakilishi wenyeviti wake wamewasilisha ripoti za kamati ambazo zimejadiliwa na wajumbe wa baraza la wawakilishi.

Kamati zilizowasilisha ripoti yake na kusomwa mbele ya wajumbe wa baraza la wawakilishi ni Ardhi na Mawasiliano, Kamati ya Habari, Utalii na Wanawake, kamati ya Ustawi wa Jamii, Kamati ya Fedha, Biashara na Viwanda pamoja na Kamati ya Ofisi ya Viongozi Wakuu wa Serikali na Kamati ya Kuchunguza na Kudhibiti Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (PAC).