Jaji Mkuu ataka wananchi waelimishwe haki

JAJI Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Hamisi Juma, amewaagiza mahakimu wa mahakama za mwanzo na wilaya nchini kuboresha utendaji wa kazi za mahakama kwa kutenga muda maalum wa kutoa elimu kwa wananchi kutambua haki zao.

Ametoa kauli hiyo katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Igunga, alipozungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Igunga katika ziara ya kikazi mkoani Tabora.

Profesa Juma amesem, mahakama ina changamoto nyingi kwa kuwa baadhi ya wananchi hawatambui namna ya kudai haki zao, hivyo ni wajibu wa mahakimu kutenga muda maalumu wa kutoa elimu kwa wananchi ili wajue haki zao za kisheria.

Amesema, elimu hiyo hata kupitia mabango kukemea vitendo vya rushwa itasaidia kupunguza msongamano wa kesi zisizo za lazima katika mahakama. Mkuu wa Wilaya ya Igunga, John Mwaipopo, alimwambia Jaji Mkuu kuwa, Wilaya ya Igunga ina wakazi wapatao 420,933 sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 2.9 kwa mwaka.

Profesa Juma amesema, kutokana na idadi kubwa ya wananchi, zinahitajika huduma zaidi za kimahakama kwa kuwa Wilaya ya Igunga ina mahakama za mwanzo 10 na moja ya wilaya wakati kiutawala zipo tarafa nne, kata 35 na vijiji 119.

Kutokana na hali hiyo, Mwaipopo alisema baadhi ya wananchi wamekuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta huduma za mahakama.

Amemwomba Jaji Mkuu kujenga mahakama za mwanzo katika kata zote 35 na endapo uwezekano huo hautakuwepo angalau ziwepo mahakama 15 za mwanzo.