Makonda aamini Polisi watatoa majibu kifo cha Akwilina

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ana imani kuwa Polisi watatoa majibu kuhusu kifo cha mwanafunzi wa Chuo Cha Taifa Cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Maftah (22).

Makonda ameyasema hayo kwenye viwanja ya NIT, Mabibo jijini Dar es Salaam wakati wa ibada ya mazishi ya msichana huyo.

Kwa mujibu wa Makonda, kifo hakizuiliki kwa kuwa ni mipango ya Mungu lakini sababu za kifo zinazuilika. Kiongozi huyo amesema, wananchi waache kunyoosheana vidole kuhusu kifo cha msichana huyo.

Wakati wa ibada hiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema serikali imelichukulia kwa uzito suala la kifo Akwilina na kwamba, Rais John Magufuli ameagiza uchunguzi ufanyike kubaini waliohusika kumuua msichana huyo.

“Natoa wito kwa vyombo vinavyohusika kuharakisha uchunguzi ili wale wote waliohusika waweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchi yetu lakini pia uchunguzi huu usaidie kudhibiti matukio ya namna hii yasiweze kujirudia,” amesema Waziri Ndalichako.

Akwilina aliaga dunia Februari 16, mwaka huu baada ya kupigwa risasi wakati akiwa ndani ya daladala, Kinondoni Mkwajuni,Dar es Salaam. Mwili wa msichana huyo unasafirishwa leo kuupeleka Rombo mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya maziko.