Kukosa taarifa za mgodi kwamkera Naibu Waziri

NAIBU Waziri wa Madini, Dotto Biteko ameonesha kukerwa na utaratibu wa uhifadhi wa takwimu za malipo ya kodi katika mgodi wa uchenjuaji wa dhahabu wa kampuni ya Sunshine wilayani Chunya mkoani Mbeya. Biteko alionesha hali hiyo baada ya kutembelea mgodi huo na kubaini udhaifu huo.

Naibu Waziri aliuliza taarifa ya ulipaji kodi, maofisa waliokuwepo eneo la mgodi, wakadai kutokuwa nazo na kwamba maofisa wa ngazi za juu wa kampuni hiyo, ambao ni raia wa China, ndiyo wanazo kwenye kompyuta yao ambayo waliifungia siku chache kabla ya kwenda kwao China.

Baadhi ya maofisa waliokutwa katika mgodi huo, ambao ni raia wa Tanzania, Mahus Ari aliyejitambulisha kama Ofisa Rasilimali watu na Lusajo Mwakabungwe, aliyesema ni Ofisa Mawasiliano wa kampuni, walidai wachina wamefungia kompyuta mpakato, iliyo na taarifa ya namna gani kampuni inalipa kodi ya serikali.

Walisisitiza kuwa wao hawajui lolote. Maofisa hao pia walijichanganya, baada ya taarifa zao kushindwa kueleza dhahiri juu ya madai ya kampuni ya kuwa mashapo ya dhahabu yaliyopo eneo la Itumbi, yamekwisha. Kwamba hiyo ndiyo sababu kampuni haiendelei na uzalishaji.

Pia walidai teknolojia waliyo nayo ni dhaifu na haiwezi kupata mashapo yaliyopo chini zaidi. Aidha, maofisa hao walimueleza naibu waziri kuwa huenda taarifa za kodi anazo raia wa China, aliyejulikana kama Mr Gun, mhasibu wa kampuni hiyo ya Sunshine.

Mtu huyo hakuwepo ukumbini hapo na ilidaiwa alikuwa amejipumzisha chumbani kwake. Naibu waziri aliagiza mhasibu huyo aitwe, lakini ofisa wa kwanza aliyetumwa kumuita, alirejea bila jibu.

Ikabidi atumwe ofisa wa pili wa kampuni hiyo kumfuata, lakini naye pia hakukuwa na jibu. Muda wote huo msafara wa Naibu waziri haukujua cha kufanya.

Baada ya dakika chache kupita, Naibu waziri alimfuata Gun chumbani kwake na kumlazimisha kwenda nae ukumbini, akatoe majibu ya takwimu za ulipaji kodi.

Hata hivyo, mhasibu huyo naye alionekana hakuwa na taarifa yoyote, ambapo kwanza aliomba apewe dakika tano ajipange. Lakini, dakika hizo tano zilipoisha, alikuwa hana sehemu ya kutoa hesabu hizo.

Biteko aliitaka kampuni hiyo kutoendelea kutangaza kuwa eneo walilokuwa wakitoa mashapo limeishiwa.

Alisema iwapo ni kweli eneo hilo limeishiwa, waoneshe namna gani wamefungia mgodi huo kwa taratibu zinazopaswa kufuatwa, ikiwemo kurejesha eneo husika katika muonekano wa awali.