Miti 100,000 kupandwa Kilimanjaro

MITI 100,000 inatarajiwa kupandwa mkoani Kilimanjaro kwa lengo la kulinda na kuhifadhi mazingira na pia kama sehemu kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani, itakayoadhimishwa mwezi Aprili mwaka huu.

Upandaji miti huo utafanywa na serikali kwa kushirikiana na taasisi ya Kilimanjaro Project na kampuni ya TBL Group.

Uamuzi huo ulitangazwa katika mkutano wa waandishi wa habari katika ofisi za TBL jijini Dar es Salaam jana na kuhudhuriwa na wawakilishi wa kampuni hiyo na taasisi ya Kilimanjaro Project.

Mkurugenzi wa Masoko Afrika Mashariki wa TBL Group, Thomas Kamphuis, alisema kwenye mkutano huo kuwa

“Mamilioni ya miti inakatwa kila mwaka mkoani Kilimanjaro pia hekari zipatazo 300,000 za ardhi zinakatwa miti kwa ajili ya mkaa na kuni na shughuli nyinginezo za kilimo, takwimu hizi zinatoa tahadhari kuwa tunapaswa kuchukua hatua ya kulinda mazingira.” Mwasisi na Kiongozi wa Mradi huo, Sarah Scottt wa taasisi ya Kilimanjaro Project alisema:

“Maandalizi ya kufanikisha mpango huu yamekuwa yakifanyika kwa miezi 6 na yanaendelea vizuri, hatua za awali za kuotesha mbegu za miti na kuainisha maeneo ya kupanda miti na mikakati ya kuitunza ili isitawi yanaendelea vizuri.”

Mradi huo kwa upande wa TBL Group, utatekelezwa na chapa yake ya bia maarufu ya Kilimanjaro Lager. Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, Pamela Kikuli alisema:

“Kupitia bia ya Kilimanjaro tutaelimisha jamii juu ya uhifadhi mazingira kuanzia kwenye mashindano maarufu duniani ya Kili Marathon yatakayofanyika Machi 4, 2018. Elimu itakayotolea itahusu uhamasishaji wa kupanda miti kwa wingi, kutunza mazingira ya asili na kuhamasisha kila mmoja kuwajibika na utunzaji wa dunia yetu tunayoishi”.

Katika miaka ya karibuni, Tanzania imekuwa ikikabiliwa na mabadiliko ya tabia nchi, ambayo yametokana na athari za uharibifu mbalimbali wa mazingira, kama vile ukataji miti ovyo na kilimo kisicho na mpangilio.

Moja ya maeneo yaliyoathirika na uharibifu huo wa mazingira ni yale yanayozunguka Mlima Kilimanjaro.