'Mliojenga ndani ya barabara Ubungo-Kimara hameni'

WAKALA wa Barabara Mkoa (Tanroads) kwa Dar es Salaam imewakumbusha wananchi waishio katika hifadhi ya barabara ya Morogoro kuanzia Ubungo Maji hadi Kimara Mwisho kuwa wasisahau kwamba wana notisi ya kuondoka maeneo hayo.

Meneja wa Tanroads wa Mkoa wa Dar es Salaam, Julius Ndyamukama alisema hayo jana wakati akizungumza na gazeti hili na kuongeza kuwa kwa sasa wakala huo amesitisha suala la kubomoa katiak eneo hilo hadi hapo baadaye.

“Tunawakumbusha wananchi waishio katika eneo hilo kuwa tayari wana notisi muda mrefu, wapo wanaofanya biashara wasiojua nini hatma yao lakini kimsingi wakumbuke kuwa hata kazi ya kubomoa ilikuwa ifanyike Desemba mwaka jana,” alisema Ndyamukama.

Hata hivyo wakala huo umesema utekelezwaji wa bomoabomoa kwa eneo hilo umesitishwa hadi baadaye. Alisema baada ya kupatiwa notisi hizo walitakiwa kuondoka katika maeneo ya hifadhi ya barabara kwa kuwa awali bomoa bomoa ilipangwa kutekelezwa Desemba mwaka jana 2017, lakini kwa sasa imesitishwa hadi baadaye (ingawaje haukuwa tayari kusema muda sahihi itakapotekelezwa).

Mmoja wa wafanyabiashara katika eneo la Kimara Korogwe, Rose Shirima alisema anapata shida kuhusu utekelezwaji wa bomoabomoa na hatma ya bidhaa zake anazouza kwa kuwa hata mwenye nyumba hasemi ukweli kuhusu suala hilo.

Alisema amejikuta akilipia pango la nyumba kwa mwezi mmoja mmoja, huku mmiliki akimuamrisha alipe kwa miezi sita, huku akiwa bado hajui endapo atalipa halafu utekelezwaji wa bomoabomoa ukafanyika.

Mkazi mwingine wa eneo la Kimara Kona ambaye ni mpangaji, Zakaria John alisema majirani wake wengi walishabomoa nyumba zao na kuondoka lakini wamejikuta wakiwa bado katika nyumba hiyo kutokana na kulipa fedha za pango la nyumba kwa muda mrefu na pindi wakitaka kuondoka hakuna aliyetayari kurudisha fedha.

Alisema kutokujua kwa hakika ni lini utekelezaji wa bomoabomoa hiyo katika eneo hilo unaweza kuathiri wengine kwa kuwa wanaweza kuwa hawapo karibu siku Wakala huo utakapoamua kutekeleza kazi hiyo.