Msajili aitwanga barua Chadema, wafuasi 28 kortini

OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, imekitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kujielezea kwa nini kisichukuliwe hatua za kinidhamu kwa ukiukwaji wa sheria na kanuni za maadili ya vyama vya siasa.

“Kwa barua hii nakitaka chama chenu kuwasilisha maelezo kwa nini msichukuliwe hatua za kisheria kwa kukiuka Sheria ya Vyama vya Siasa na Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa kwa kuchochea wananchi kuandamana bila kufuata utaratibu wa sheria na kufanya vurugu.

Maelezo haya yawasilishwe ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa siyo zaidi ya tarehe 25 mwezi Februari 2018,” alieleza Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi katika barua yake kwa Chadema, iliyotolewa jijini Dar es Salaam jana. Barua hiyo kwa Chadema ilieleza kuwa katika mkutano wa mwisho wa kufunga kampeni za uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni uliofanyika katika Viwanja vya Mwananyamala kwa Kopa, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitoa lugha za kuchochea vurugu.

Barua hiyo iliendelea kufafanua kuwa alichokifanya kinakatazwa na Kifungu cha 9(2)cha Sheria ya Vyama vya Siasa na Kanuni ya 5(1) ya Maadili ya Vyama vya Siasa. Februari 16, wanachama wa Chadema waliandamana kutokea kwenye mkutano huo wakielekea ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi ambapo wakiwa njiani zilitokea vurugu.

Wakati huohuo, Watu 28 wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka ya kufanya mkusanyiko usiokuwa halali. Baadhi ya washitakiwa hao ni Thabita Mkude, Haji Lukwambe, Mohammed Juma, Hussen Mnombo, Brian Moris, Abdallah Khamis, Fatma Ramadhan, Raphael Mwaipopo na Emmanuel Kimoyi.

Pia wapo Hussen Kidela, Salma Ngondo, Asha Kileta, Paul Kimaro, Edna Kimaro, Haji Mkwambe na Hussein Kidela. Walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa.

Wakili wa serikali, Faraji Nguka alidai washitakiwa kwa pamoja Februari 16, mwaka huu katika Barabara ya Kawawa maeneo ya Kinondoni Mkwajuni, walifanya mkusanyiko usio halali, wakiwa na nia ya kusababisha uvunjifu wa amani. Hata hivyo, Hakimu Mwambapa alitoa masharti ya dhamana kuwa kila mshitakiwa alitakiwa kuwa na mdhamini mmoja, atakayesaini bondi ya Sh milioni 1.5. Hakimu Mwambapa aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 8, mwaka huu.