UNIDO kupaisha sera ya viwanda Tanzania kimataifa

SERIKALI imesaini makubaliano na Shirika la Umoja wa Mataifa Linaloshughulikia Viwanda (UNIDO) ya kuitoa Tanzania katika mipango ya kitaifa kwenda kwenye mipango ya nchi na washirika ili kufi kia uchumi wa kati.

Makubaliano hayo yalisainiwa jijini Dar es Salaam jana na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage na Mkurugenzi Mkuu wa UNIDO, Li yong na kushuhudiwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, viongozi mbalimbali pamoja na wadau wa maendeleo. Mwijage alisema, “UNIDO itatusaidia kuona ni namna gani tutaipeleka nchi katika uchumi wa kati kupitia uchumi wa viwanda kwa kuwa wawekezaji wakubwa na wakopeshaji wakubwa ni lazima wawaulize UNIDO, hivyo hii pia inamuweka katika nafasi nzuri ya kutujua na kutuuza sambamba na kututafutia washirika”.

Alisema mambo ambayo wanatarajia kufanya kupitia makubaliano hayo ni UNIDO itakuwa na jukumu la kutafuta washirika wengine, kuja kuangalia namna gani wanaweza kusaidia katika mpango wa Taifa wa miaka mitano, ambao kwa sasa dhima yake ni ujenzi wa uchumi wa viwanda ili kufanya mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu. “Tuliyoyapanga yanakwenda kutafuta washirika ili watusaidie kutekeleza... Mpango haupangwi na UNIDO, ila unapangwa na sisi na yeye anashirikiana na mashirika ya Umoja wa Mataifa na taasisi mbalimbali na kuwaweka chini kuangalia mipango yetu tunapoelekea kwenye ujenzi wa uchumi wa viwanda,” alisema.

Mwijage alisema mambo wanayotegemea kufanywa katika mpango miaka mitano na mwingine ujao wa kuleta ushindani ni kuendelea kujenga maeneo yaliyo rasmi ya uwekezaji, miundombinu wezeshi na saidizi. Alisema “Tunapohangaika kutafuta na kuandaa wataalamu wetu yeye atatusaidia tufanye namna gani ili kuandaa wataalamu wetu wa kuendesha viwanda na wale wafundishaji, pia tutashirikiana naye kuongeza ajira hivyo shughuli zote zitalenga kuongeza thamani kuliko kuuza mali ghafi”.

Pia alisema wamelenga kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla, huku malengo makuu matatu yakiwa ni kutengeneza ajira, kuzalisha bidhaa zenye viwango vya ubora wa hali ya juu na kuwapatia watu kipato kuanzia wanaoshiriki shambani hadi viwandani. Hata hivyo, alisema watatengeneza wigo wa ulipaji kodi, utakaosaidia mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu ikiwemo afya, elimu na kipato ili kuiwezesha nchi kufikia uchumi wa kati.

Yong alisema kuwa wataisaidia Tanzania katika mpango wa miaka mitano, ikiwemo kukuza sekta ya viwanda, ajira kwa wanawake na vijana na utunzaji wa mazingira. Katika mazungumzo yake na Makamu wa Rais, Mkurugenzi alisema anajua Tanzania ina ajenda kuu ya uanzishwaji wa viwanda. Alimhakikishia Makamu wa Rais kwamba UNIDO itajitahidi kusaidia ajenda hiyo.