Polisi yachunguza kutekwa kwa mwanafunzi UDSM

JESHI la Polisi Mkoa wa Iringa limeanza kufanya uchunguzi wa tukio la kutekwa kwa Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo ambaye pia ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Kitivo cha Siasa na Utawala cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Aidha, limesema kuwa kama itabainika kuwa taarifa za kutekwa kwake ni za uongo, mwanafunzi huyo atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi. Mwanafunzi huyo anadaiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha Jumanne usiku akiwa jijini Dar es Salaam na alionekana asubuhi ya Jumatano ya Machi 7, mwaka huu mjini Mafinga wilayani Mufindi mkoani Iringa baada ya kwenda kutoa taarifa hiyo Polisi.

Jana majira ya saa 4.45 asubuhi, mwanafunzi huyo alifikishwa makao makuu ya polisi mkoani Iringa akiwa katika gari dogo binafsi aina ya Toyota Porte, lenye namba za usajili T 256 DDW akiwa chini ya ulinzi wa maofisa wa polisi watatu akitokea Kituo cha Polisi cha Mafinga. Akizungumza na wanahabari kwa sharti la kutoulizwa swali lolote ili kutovuruga uchunguzi wa tukio hilo jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Juma Bwire alisema mwanafunzi huyo alifika katika kituo kidogo cha Polisi cha mjini Mafinga juzi Jumatano majira ya saa 1.00 asubuhi na kueleza kwamba alitekwa na watu wasiojulikana.

Alisema Jeshi la Polisi limefungua jalada la uchunguzi na limejipanga kuchukua hatua stahiki, ikiwemo ya kuwasaka na kuwafikisha katika vyombo vya dola, watuhumiwa watakaobainika kuhusika na tukio hilo. Bwire alisema kama atakuwa ametoa taarifa za uongo kwa nia ovu, ikiwemo ya kutaka kuwahamasisha wanafunzi wenzake kuvunja amani, mwanafunzi huyo atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

“Tunaendelea kumhoji mwanafunzi huyu na kama mnavyomuona mbele yenu hali yake ni nzuri, hana majeraha wala makovu na afya yake ni nzuri,” alisema. Mbali na yeye kukataa kujibu maswali ya wanahabari, Kamanda Bwire alizuia pia mwanafunzi huyo kuulizwa swali lolote, akisema hiyo itasaidia kutovuruga uchunguzi unaoendelea. Aliwaomba wananchi wenye taarifa zozote, zinazohusiana na tukio hilo, kujitokeza kutoa ushirikiano ili kukamilisha suala hilo kwa wakati.