Kinapa kutumia Marathon kutangaza mti mrefu Afrika

HIFADHI ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro, (Kinapa), inakusudia kuzitumia mbio za Kili Marathon zinazofanyika kila mwaka mkoani Kilimanjaro, kutangaza zaidi vivutio vya utalii vilivyopo sanjari na mti mrefu, kuliko yote barani Afrika uliogundulika ndani ya msitu wa hifadhi hiyo.

Mti huo wenye urefu wa mita 81.5 uliogunduliwa na wanasayansi na watafiti wa masuala ya mazingira na viumbe hai kutoka Chuo Kikuu cha Bayreuth cha nchini Ujeruman, Dk Andreas Hemps na Dk Claudia Hemps, unakadiriwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 600.

Mhifadhi Ikolojia wa Kinapa, ambaye pia ni Kaimu Mhifadhi Mkuu wa hifadhi hiyo, Iman Kikoti alisema hayo katika mahojiano maalumu baada ya kumalizika kwa mbio hizo wiki iliyopita zilizobeba jina la Mlima Kilimanjaro ambao ni mrefu kuliko yote barani Afrika. Mti huo unaopatikana katika eneo la Mrusungu ndani ya Hifadhi ya Kinapa yenye urefu wa takriban mita 1,600 kutoka usawa wa bahari umegundulika baada ya utafiti huo kuhusisha pia miti mingine katika nchi nyingine barani Afrika.