Walimu 560 wa masomo ya sanaa sekondari wahamishiwa msingi

WALIMU 560 waliokuwa wakifundisha masomo ya sanaa katika shule za sekondari mkoani Kagera, wamepelekwa kufundisha katika shule za msingi mkoani humo, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Ofi si ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Ofisa Elimu wa Mkoawa kagera, Aloyce Kamamba, alibainisha hayo alipozungumza na vyombo vya habari mjini Bukoba. Alisema baada ya kupokea taarifa kutoka Tamisemi - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera ilifanya taratibu za kuwabaini walimu wa ziada kutoka shule za sekondari ndani ya wilaya nane za mkoa huo.

Alisema hadi hivi sasa tayari Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo imepewa walimu 15, Halmashauri ya Bukoba 44, Manispaa ya Bukoba 44, Halmashauri ya Muleba 186, Halmashauri ya Ngara 40, Halmashauri ya Misenyi 111 na Halmashauri ya wilaya Karagwe 117.