JPM: Sitatoa fedha tena kusaidia benki

RAIS John Magufuli amesema kuanzia sasa serikali haitatoa fedha kuzisaidia benki zinazosuasua katika kujiendesha kama ilivyozoeleka, hata kama benki husika zina mitaji ya serikali.

Aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa Tawi la Benki ya CRDB mjini Chato mkoani Geita na kusema kuwa benki ni kama biashara nyingine na hivyo zinapofanya vibaya hata kama utakuwa na mtaji wa serikali lazima zitakufa tu. “Ndio nasema hapa leo sitatoa tena fedha za wananchi kwa ajili ya kuokoa benki yoyote, hata kama ni benki ya wanaume, wanawake, watoto, CCM au serikali… CRDB benki anzeni kuangalia vibenki vinavyosusua muungane navyo kuviinua,” alisema.

Alitoa wito kwa benki zinazosuasua kujiunga na benki kubwa zilizo imara ili ziweze kuwa na nguvu za kujiendesha na benki kubwa ziwe tayari kuzipokea benki hizo ndogo na kuzikwamua kibiashara kama zimeshindwa kusimama zenyewe. Rais Magufuli alieleza kukerwa na tabia za benki ambazo zinashindwa kujiendesha kibiashara, halafu zinasubiri kusaidiwa na serikali na kisha zinaposaidiwa badala ya kujiinua, zinatumia fedha zilizopewa vibaya.

“Kuna tabia ya baadhi ya benki hazifanyi biashara, halafu zinasubiri kufilisika zinajua serikali itasaidia, hizi ni fedha za wananchi ambazo tungezitumia kujenge shule, miradi ya maendeleo na miradi mingine ya manufaa kwa wananchi. “Halafu zikipewa fedha badala ya kujiendesha ili ziinuke, wanatumia kwa masuala yao binafsi na wengine hadi kukopeshana… sasa hata kama ni benki ya serikali acha ife tu, sitatoa tena fedha kusaidia benki hizo,” alisema.

Alisema; “Katika benki hizo zinazosuasua ndiko ‘majizi’ walikuwa wanakopa halafu hawarudishi mikopo na mwisho wake benki zinashindwa kujiendesha kibiashara na matokeo yake zinafilisika zikiwa na matuamini ya kusaidiwa na serikali. Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alitoa wito kwa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kuendelea kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuzifungia benki ambazo zinaendeshwa kwa kusuasua ili kulinda sekta ya benki na uchumi wa nchi. Sambamba na hilo, Rais Magufuli alipongeza BOT kwa kuzifungia benki tano na kuziwekea muda wa matazamio wa miezi sita benki nyingine tatu ambazo zinaendeshwa kwa kusuasua.

Rais Magufuli alitoa wito kwa Benki ya Kuu Tanzania (BOT) kuchukua hatua kwa benki zote ambazo zinashindwa kujiendesha kibiashara na kuongeza kuwa ni heri kuwa na benki chache zenye nguvu kama CRDB zinazohudumiwa wananchi kwa ufanisi kuliko kuwa na utitiri wa benki zinazojikongoja. “BOT muanze kuzichukulia hatua benki zote zinazojikongoja na kuzimaliza zote, najua kuna watu watasema, lakini sisi tunafanya kwa niaba ya wananchi masikini ambao tunatumia fedha zao halafu kwenye benki wanazichezea badala ya kufanya biashara… hakuna faida ya kuwa na benki 100 zinazosuasua bora kuwa nazo chache zinazotoa huduma bora kwa wananchi,” aliongeza Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine Rais Magufuli alitoa wito kwa BOT na benki nyingine kupunguza riba ili wananchi masikini waweze kuweka mitaji yao katika benki hizo. “Najua Mkurugenzi Kimei, CRDB inaoongoza katika mabadiliko ya sekta ya kibenki lakini pia nimesikia wewe ni kiongozi wa viongozi wa mabenki naomba mkizungumza huko muone hili la kupunguza riba zenu ili wananchi wasiogope kuzitumia,” alisema. Alisema ni asilimia 16.7 tu ya Watanzania ndio wanaohudumiwa na benki wakati idadi ya Watanzania ni kati ya milioni 54 na kuitaka BOT na benki nyingine kupunguza riba ili kuendana na dhana ya Tanzania ya Viwanda.

Alitoa wito kwa wananchi wa Chato na Watanzania wote kwa ujumla kutoziogopa benki na badala yake wazitumie ili kupata huduma mbalimbali za kibenki ikiwemo kukopa huku akisisitiza dawa ya kukopa ni kulipa. Rais Magufuli alitoa mfano kuwa serikali ilikuwa inadaiwa Sh bilioni 16 na CRDB lakini wamelipa fedha hizo na kuongeza kuwa zilikuwa kwa ajili ya mbolea, kwa hiyo hata kama mbolea haikupelekwa haijalishi kwani dawa ya deni ni kulipa deni. Aliwaomba Watanzania kuwa wazalendo na kuiunga mkono serikali katika masuala mbalimbali inayofanya kuleta maendeleo.

Aliwahakikishia Watanzania kuwa nchi inakwenda vizuri na aliwataka kuunga mkono hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali ambazo zimeanza kuimarisha uchumi na kuwezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo kama vile ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge), uzalishaji umeme katika maporomoko ya Mto Rufiji (Stieglers Gorge), ununuzi wa ndege sita, ujenzi wa barabara na madaraja na hivi karibuni serikali itasaini mkataba wa ujenzi wa meli katika Ziwa Victoria itakayogharimu Sh bilioni 35. “Naomba Watanzania tuwe wazalendo kwa kuunga mkono juhudi mbalimbali tunazofanya.

Unajua mtu siku zote anayefanya vizuri lazima achukiwe… unadhani hivi tunavyofanya miradi mikubwa kama mradi wa Standard Gauge wapo wasiofurahi, lakini sisi tuwe wazalendo tupende maendeleo yetu,” alisema. Aidha, aliwataka Watanzania kutokubali kutumiwa katika vitendo vya uvunjifu wa amani ambavyo vinaweza kusababisha machafuko kama yaliyotokea kwa nchi jirani na nyingine duniani, na kuonya kuwa vyombo vya dola havitawavumilia watakaothubutu kuvunja sheria na kuleta vurugu.

Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo, Ally Laay na Mkurugenzi Mtendaji Charles Kimei walisema CRDB imeendelea kufanya vizuri ambapo katika miezi mitatu iliyopita amana zimeongezeka kutoka Sh trilioni 4 hadi 4.4, imeanzisha bidhaa iitwayo “Kilimo Fahari” yenye lengo la kuwakopesha wakulima, na inatarajia kuwaunganisha wafanyabiashara wa Tanzania na wawekezaji wakubwa wa viwanda kutoka nchi zenye teknolojia na mitaji mikubwa zaidi ili kuendeleza viwanda nchini.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji alisema Tanzania inafanya vizuri katika mpango wa fedha jumuishi ambapo katika miaka tatu mfululizo imeshika nafasi ya kwanza Barani Afrika na nafasi ya sita duniani na kwamba juhudi zinaendelea kufanywa ili kuongeza idadi ya Watanzania wanaotumia huduma za kifedha.