Mahakama yatupa ombi kesi ya muungano kufanyika Zanzibar

MAHAKAMA ya Afrika Mashariki (EACJ) imelifutilia mbali ombi la kutaka kesi iliyowasilishwa katika mahakama hiyo, kuhusu uhalali wa Muungano ikafanyikie Zanzibar.

Hukumu ya Mahakama hiyo kuamua kufuta kesi (0mbi) namba saba(7) ya mwaka 2017, ilitolewa siku ya Alhamisi na Jaji Monica Mugenyi baada ya kujiridhisha kwamba, mleta ombi alikuwa amekiuka baadhi ya vifungu vya sheria katika uwasilishaji wa ombi lake.

Mleta maombi Rashid Salum Adiy anayewawakilisha wengine 39,999, alitaka kesi kuhusu uhalali wa Muungano ikasikilizwe Zanzibar, huku akimtambulisha mbele ya mahakama hiyo Japhet Chigumba kwamba ndiye atakayewawakilisha upande wa wawaleta maombi pasipo kukidhi vigezo vya kisheria.

Baada ya makahama kulikataa ombi la kuletwa kwa Wakala huo, mleta ombi Rashid Salum Adiy aliiomba mahakama iendelee na shauri hilo peke yake na atumie lugha ya kiswahili, ombi ambalo pia lilikataliwa.

Upande wa utetezi ( Jamhuri) uliwakilishwa na Mzee Ali Haji, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Alesia A. Mbuya, Wakili Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mark Mulwambo, Wakili wa Serikali Mwandamizi naye aliiomba Mahakama kulifutilia mbali ombi hilo kutokana na mwasilishaji kukosea baadhi ya vifungu vya sheria kikiwamo kifungu 47(1)(a)na (c) Kanuni za Mahakama ya Afrika Mashariki za Mwaka 2013.

Wakili Mkuu wa Serikali, Alesia Mbuya, aliieleza mahakama hiyo kwamba mleta ombi alikuwa amekiuka kifungu cha sheria hiyo kwa kuwasilisha jina la wakala bila ya kuzingatia matakwa ya kisheria na kuwa mleta ombi, alikuwa anafanya makusudi kwa lengo la kuchelewesha usikilizwaji wa kesi ya msingi lakini pia ni kuitumia vibaya mahakama hiyo.

Jaji aliyesikiliza ombi hilo Monica Muganyi akisaidiwa na Majaji Fakihi Jundu na Dk Chales Nyawella, alikubaliana na upande wa wajibu maombi kwamba mleta maombi alikuwa amekosea vifungu vya sheria na hivyo kulifutilia mbali ombi hilo.