JPM: Tuwe wazalendo

RAIS John Magufuli amewataka wakandarasi wazawa wanaopata kazi katika miradi mbalimbali inayotolewa na serikali, kuhakikisha kuwa wanatumia bidhaa za ndani kabla ya kutumia bidhaa za nje.

Rais Magufuli aliyasema hayo jana, wakati akifungua kiwanda cha kutengeneza mabomba ya plastiki, mabati pamoja chuma kinachomilikiwa na Kahama Oil Mill kilichopo Mjini Kahama. “Ukitumia bidhaa za ndani unasaidia kutengeneza ajira kwa wazawa kuliko unapotumia bidhaa za nje ambapo unakuwa unatengeneza ajira kwa watu wa nje, hivyo wamiliki wa viwanda vinavyotengeza bidhaa tengenezeni kwa ubora unaotakiwa ili kulinda soko la ndani,” alisema.

Alisema, kila mkandarasi hapa nchini anatakiwa kutumia bidhaa zinazotengenezwa hapa nchini katika shughuli zake na kuongeza kuwa bidhaa zinapoisha na shughuli zake bado zinaendelea anatakiwa kupata kibali cha kuagiza bidhaa kutoka nje. “Kila Mtanzania anatakiwa kuwa mzalendo kwa kupenda cha kwake na siyo kupenda bidhaa zinazotengenezwa nje hali ambayo haiwezi kuongeza ajira kwa Watanzania na kukuza uchumi wa nchi, badala yake tunakuwa tunawatengezea ajira watu wa nje,” alisema Magufuli.

Hata hivyo alizitaka taasisi za fedha zikiwemo benki kuhakikisha zinapunguza riba kwa wafanyabiashara na kuongeza kuwa awali mabenki mengine yalikuwa yanatoza riba kubwa mpaka asilimia 25 hali ambayo wawekezaji wa viwanda wanashidwa kujiendesha na kujikuta yanapata hasara huku akisema kwa sasa jumla ya viwanda 3600 tayari vimekwisha funguliwa nchini.

Wakati huo huo, Rais Magufuli aliwataka wawekezaji kutumia malighafi zinazopatikana hapa nchini hususani madini ya chuma hali itakayowafanya kuzalisha bidhaa zao kwa faida kubwa kuliko kuendelea kutumia malighafi kutoka nje. Mkurugenzi wa Kiwanda cha Kahama Oil Mill, Mhoja Nkwambi alisema kuwa kiwanda hicho kilianzishwa mwaka 2002 nakutoa ajira 720 huku 120 zikiwa ajira za kudumu na 600 zikiwa ajira za muda mfupi kulingana na upatikanaji wa malighafi.

Alisema, amekuwa akipata changamoto za uuzaji wa bidhaa anazozalisha kutokana na bidhaa zinazotengenezwa nje kuingia kwa wingi nakupelekea bidhaa zinazotengezwa ndani kukosa soko hata kama zinakidhi ubora. Nkwambi alisema serikali ithamini bidhaa zinazotengenezwa ndani badala ya kutoa kipaumbele kwa bidha zinazotoka nje ya nchi na kuvilinda viwanda vya ndani ili viweze kujiendesha na kupata mikopo ya riba fuu kutoka katika mabenki na tasisisi mbalimbali za kifedha.

Pia Mkurugenzi huyo aliiomba serikali kumsaidia kupata soko la mabomba ya plastiki, mabati na vyuma hapa nchini ili wanunuzi waache kuagiza bidhaa hizo kutoka nje na kwamba, hali hiyo itasida kuvilinda viwanda katika ushindani wa kibishara katika masoko ya ndani na nje.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack kujipanga katika kuleta wanunuzi wa zao la Pamba watakaonunua zao hilo katika msimu huu kwa bei nzuri. Rais Magufuli aliyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Mji wa Kahama katika uzinduzi wa barabara ya kilometa 132 inayotoka katika mji mdogo wa Isaka hadi Rusahunga iliyopo Mkoa wa Kagera.

Alisema, watu wamelima kwa wingi zao hilo ambalo lilikuwa likionekana kuwakatisha tamaa wakulima katika kipindi cha nyuma kutokana na bei ya zao hilo kuwa chini na baadhi ya kampuni zilizokuwa yakijishughulisha na ununuzi wa pamba kuwadhulumu fedha zao.

“Ninaiomba Serikali ya Mkoa wa Shinyanga katika msimu huu wa kilimo cha pamba kuhakikisha kuwa inajipanga katika kutafuta wanunuzi watakaonunua pamba ya wakulima kwa bei nzuri ili kilimo anachokiendesha mkulima wa Pamba kiwe ni kilimo chenye tija ambacho kitamuinua mkulima kiuchumu,” alisema.

Taleck pamoja na mambo mengine alimweleza Rais Magufuli kuwa Halmashauri ya Mji wa Kahama imetenga kiasi cha Sh bilioni 2.1 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri hiyo na kwamba fedha hizo ni ndogo. Pia alisema kuwa imetenga kiasi cha ekari 22 kwa ajili ya kuwavutia wawekezaji kuwekeza katika mji huo ambao kwa kiasi kikubwa umekuwa na watu wengi ambao hawana ajira rasmi.