Mpina apewa rungu uchomaji nyavu haramu

RAIS John Magufuli amemtaka Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina kuendelea kuchoma nyavu haramu, zinazotumika kwa shughuli za uvuvi katika Ziwa Victora.

Amesema hatua hiyo itawezesha samaki wengi zaidi, wazaliane katika ziwa hilo. Akizungumza mjini Chatomwishoni mwa wiki kwenye uzinduzi wa tawi la Benki ya CRDB, Rais Magufuli alisema kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Waziri Mpina ya kuteketeza zana haramu za uvuvi, sasa samaki wameanza kuongezeka katika Ziwa Victoria. Aliongeza kuwa awali wavuvi walikuwa wakivua samaki wachanga, hivyo ni lazima hatua kali ziendelee kuchukuliwa ili kudhibiti uvuvi haramu ili rasilimali hizo ziweze kunufaisha kizazi cha sasa na kijacho.

“Ninawapongeza sana wananchi wa Chato kwa kuendelea kupiga vita uvuvi haramu na kwa hili nampongeza sana Waziri Mpina …endelea kuchoma makokoro ili kusudi samaki wengi waanze kuzaliana na kwa ninyi wa Chato, nafikiri ni mashahidi sasa hivi samaki zinazovuliwa ni kubwa kubwa, nasema uongo?” alisema Rais Magufuli.

Wananchi waliohudhuria mkutano huo, walimhakikishia Rais Magufuli kuwa kweli samaki wameanza kuongezeka katika Ziwa Victoria kutokana na operesheni kali, iliyofanyika mwanzoni mwa mwaka huu ya kupambana na uvuvi haramu. “Samaki zimeanza sasa kwa sababu tulikuwa tunavua samaki ambazo hazizai, lazima tubanane katika kuleta maendeleo ya nchi yetu,” alisisitiza Rais Magufuli.

Pamoja na Rais Magufuli kukazia vita dhidi ya uvuvi haramu tayari nchi Tanzania, Kenya na Uganda kwa pamoja zimeridhia kufanya operesheni ya pamoja ya kupambana na uvuvi haramu katika Ziwa Victoria ili kuokoa samaki aina ya sangara, walioko katika hatari kubwa ya kutoweka.

Uamuzi huo ulifikiwa na Baraza la Mawaziri wa Sekta ya Uvuvi Kanda ya Ziwa Victoria (LVFO), ambapo wameidhinisha Dola za Marekani 1,800,000 sawa na Sh bilioni 4.1 kwa ajili ya kufanya operesheni hiyo katika Ziwa Victoria. Nchi za Kenya, Uganda na Tanzania, kila moja itapata Dola za Marekani 600,000 sawa na Sh bilioni 1.3 ili kufanikisha operesheni hiyo ya kuokoa samaki walioko katika tishio la kutoweka katika Ziwa Victoria kutokana na kushamiri uvuvi haramu.