Waziri asisitiza kuna fursa tele Zanzibar

WAZIRI wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mahmoud Thabit Kombo amewataka wananchi kuchangamkia fursa mbalimbali zinazohusu utalii wa mambo ya kale, ambao asilimia 80 ya mambo yake hayajulikani.

Alibainisha kuwa mambo ya kale, kama Mji Mkongwe na mengineyo, ambayo watalii wanafika na kuona ni asilimia 20 pekee. Waziri huyo alisema hayo wakati akielezea namna fursa mbalimbali, zinazoweza kuongeza kipato na kukuza uchumi wa visiwa hivyo, ikiwemo mambo ya kale, habari na utalii.

Alisema yeye mwenyewe, baadhi ya mambo ya kale hayafahamu, kwani mambo ya kale ndiyo utambulisho, asili ya mtu siyo kitambulisho, bali historia ya mtu ndiyo asili yake na utaifa. “Jana nilikuwa napitia ripoti niliyokabidhiwa baada ya kuingia wizarani nikaona jinsi gani mambo ya kale nilikuwa siyafahamu, mambo ya kale ndiyo thamani ya utu wetu, ndiyo utambulisho wetu,” alisema.

Anaeleza kuwa historia ya mtu, asili ya mtu, anakotokea ndiyo utambulisho wake siyo kitambulisho kinachobebwa, utaifa na uzalendo unatokana na historia na asili ya mtu anapotokea.

Waziri alisema katika historia kuna utamaduni, vyakula, muziki na kila aina ya mwenendo hata kivazi. Alibainisha kuwa katika mambo hayo, ndipo fursa nyingi zinaweza kuibuka, kwani hata watalii wengi wanaenda pwani ya bahari na maeneo machache, hawajaangalia maeneo mengi ya kihistoria, wanajua mji mkongwe na maeneo mengine machache. Alisema katika kutangaza fursa hizo, watatoa machapisho na kazi kubwa ya kutangaza nchi, maendeleo utalii, kifedha, kimapato ni kazi ya waandishi wa habari, kwani wana nguvu kwa kufanya nchi zibadilike kwa kutangaza kwa mataifa mbalimbali. Waziri alieleza kuwa inatakiwa kuandaa Jukwaa kwa ajili ya mambo ya kale, kwa kuwaita wataalamu wa masuala uchimbuaji na wengine, kwani historia ya Zanzibar ipo mpaka ya mwaka 1500 ambapo kuna vikombe, sahani na maandishi vimepimwa ni vya miaka hiyo.