Naibu Waziri: Watanzania milioni 1.7 hawaoni vizuri

Tanzania inakadiriwa kuwa na watu million 1.7 wenye matatizo ya kutokuona vizuri. Hata hivyo, watu milioni 253 wanakabiliwa na matatizo hayo duniani, kati yao, milioni 36 hawaoni kabisa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile, matatizo ya macho yanayoongezeka ni mtoto wa jicho, tatizo la upeo mdogo wa macho kuona na shinikizo la macho.

Naibu Waziri amesema hayo kuelekea wiki ya maadhimisho ya elimu ya ugonjwa wa shinikizo la macho itakayotolewa kuanzia Machi 11 mpaka 17, mwaka huu katika hospitali mbalimbali hapa nchini.

“Ugonjwa wa shinikizo ni moja ya kundi la magonjwa ya macho yanayoshambulia mshipa wa fahamu unaopeleka mawasiliano ya uoni kwenye ubongo ili kuweza kutafsiri kile unchokiona. Ugonjwa huu husababisha upofu taratibu sana, kuna umuhimu wa kupima macho angalau mara moja kila mwaka,” ameshauri Dk Ndugulile.