TSN, Data Lab kushirikiana matumizi habari za takwimu

KAMPUNI ya Magazeti ya Serikali ya Tanzania Standard Newspapers (TSN) na mradi wa Tanzania Data Lab wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Shule ya Tehama, zimeazimia kushirikiana kuongeza wigo wa matumizi ya habari za takwimu kutoa taarifa mbalimbali za kijamii hasa utekelezaji wa mkakati wa Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

TSN ni kampuni inayochapisha magazeti ya HabariLeo, HabariLeo Jumapili, HabariLeo Afrika Mashariki, Daily News, Sunday News na SpotiLeo. Mhariri Mtendaji wa TSN, Dk Jim Yonazi aliyasema hayo juzi alipokuwa akifunga semina ya siku mbili kwa wanawake wa sekta binafsi na umma, iliyohusu namna ya kutoa taarifa kwa jamii kwa njia ya data. Dk Yonazi aliwakilishwa na Mkuu wa Kitengo cha Utafiti, Ubunifu na Machapisho cha TSN, Ichikaeli Maro.

Alisema ulimwengu wa taarifa na habari wa leo unategemea zaidi data na hata lengo la kufikia 50/50 katika nafasi za uongozi ifikapo 2030 linahitaji data sahihi kulieleza ili lieleweke kwa jamii. Kuhusu kushirikiana, Dk Yonazi alisema TSN ina uzoefu mkubwa katika kuandika habari za takwimu kwani imeendesha mafunzo kwa baadhi ya wafanyakazi wake na wana weledi na ukuzi mkubwa katika eneo hilo na ushirikiano huo utaongeza matokeo chanya kwa jamii.

Akitolea mfano, alisema moja ya habari iliyoleta matokeo chanya baada ya kuanza kutumia data katika habari ni hali mbaya ya shule kongwe za serikali na namna zinavyoweza kurejeshwa kwenye ubora wake na kuongeza kuwa habari hiyo baada ya kuandikwa gazetini kwa mfumo wa data, serikali ilichukua hatua mara moja. Naye Mkurugenzi wa Tanzania Data Lab, Dk Godfrey Justo, alisema wapo tayari kushirikiana na TSN katika kutoa habari zenye data kwani katika mafunzo hayo wamegundua ndio njia bora na ya kueleweka zaidi katika kufikisha taarifa kwa wananchi.