Mbarawa aialika Rwanda kutumia ofisi za TPA

SERIKALI ya Rwanda imesema ina matumaini makubwa ya kuboresha biashara baina ya nchi hiyo na Tanzania kufuatia hatua yaMamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kufungua rasmi ofi si jijini Kigali, Rwanda, na hivyo kuileta bandari ya Dar es Salaam nchini mwao.

Waziri wa Miundombinu wa Rwanda, James Musoni alisema katika hotuba yake wakati wa uzinduzi wa ofisi hiyo kwamba anaamini hatua hiyo itapunguza gharama za wafanyabiashara wa Rwanda ambao sasa hawatalazimika tena kuwa wanasafiri hadi Dar es Salaam, Tanzania. Hafla ya uzinduzi wa ofisi hiyo mpya iliyohudhuriwa pia na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wa Tanzania, Profesa Makame Mbarawa na Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Ali Iddi Siwa, ilifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita jijiji Kigali.

Alisema hatua ya TPA kufungua ofisi Kigali ni muhimu hasa kwa kuzingatia kwamba ndani ya miaka miwili, mzigo wa Rwanda unaopitia Tanzania umeongezeka kwa asilimia 80 huku kipindi cha mzigo kukaa bandarini kikipungua hadi siku nane, hatua iliyopunguza gharama pia. Kwa sasa, Rwanda inakadiriwa kusafirisha tani 950,000 za mzigo kwa mwaka, kiasi ambacho kinatarajiwa kupaa zaidi baada ya kufunguliwa kwa ofisi na hivyo kutengeneza urahisi zaidi wa mchakato mzigo wa usafirishaji wa mzigo.

Musoni pia alipongeza hatua inayoendelea ya kujenga bandari kavu Isaka, mkoani Shinyanga ambapo mizigo ya Rwanda itakuwa inahifadhiwa kabla ya kuchukuliwa baada ya taratibu kukamilika. Umbali wa kutoka Isaka hadi Rusumo kwenye mpaka wa Tanzania na Rwanda ni kilometa 338 kwa njia ya barabara.

Waziri Mbarawa aliwataka wafanyabiashara wa Rwanda kutumia ofisi hiyo mpya ya TPA jijini Kigali kupata taarifa sahihi kuhusu usafirishaji mizigo kupitia Tanzania na kufanya malipo kupitia ECO Bank ya jijini Kigali. Alisema ujio wa ofisi hiyo ulitokana na makubaliano yaliyofikiwa baina ya Rwanda na Tanzania Oktoba 27 mwaka jana yaliyolenga kuboresha zaidi mahusiano ya biashara ya kibandari baina ya nchi hizo.