Mwakyembe awaasa maofisa mawasiliano

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ametoa rai kwa maofi sa habari na mawasiliano kutangaza habari za halmashauri, taasisi mchini kupitia tovuti badala ya tovuti hizo kugeuka magofu.

Aidha ametoa rai kwa viongozi katika hamashauri zote nchini na taasisi kushirikiana na maofisa habari kuhakikisha wanazisemea vyema taasisi zao badala ya kuwa genge la kuisema serikali bila ya uhakika wa jambo kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT). Alisema hayo alipokuwa anafungua Kikao cha siku tano cha Maofisa Habari na Mawasiliano 300 kutoka Halmashauri zote nchini chenye kaulimbiu ya “Je? Mawasiliano ya Kimkakati yanachagiza vipi Tanzania ya Viwanda”.

Akizungumza katika mkutano huo ambao Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) inayochapisha gazeti hili na magazeti dada ya HabariLeo, HabariLeo Jumapili, Daily News, Sunday News na Spoti Leo imedhamini, Dk Mwakyembe alisema ofisa habari bora ni yule anayejituma kwa kufanya kazi zake vizuri ikiwemo kupata vifaa vya kufanyia kazi na kuwasisitiza kuwa enzi za mizaha zimeshapitwa na wakati hivyo ni vyema wakachapa kazi tu.

Pia Waziri Mwakyembe kwa utafiti alioufanya kupitia kwa wasaidizi wake alisifu Halmashauri tisa zinazohuisha taarifa zake kwa wakati kupitia tovuti zao akizitaja kuwa ni Kishapu, Mtwara- Mikindani, Mufindi, Mlele (Katavi), Kinondoni, Ilala, Ubungo na Kibaha (Pwani). Aliitaja Mikoa 18 inayofanya vyema kwa kuhuisha taarifa zake ikiwemo Mwanza, Mara, Kagera, Shinyanga, Kigoma, Tabora, Simiyu, Tanga, Arusha, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Morogoro, Katavi, Geita, Songwe, Rukwa, Mbeya zinazoongoza kutoa taarifa za mikoa. Alisema pia kuwa zipo wizara tatu ambazo haziweki taarifa zake kwenye tovuti wala kutangaza kazi zake na kuwa atasema hilo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ajue la kufanya.