Mapendekezo ya mipango, bajeti ya serikali bungeni leo

SERIKALI inawasilisha mbele ya wabunge wote mapendekezo ya serikali ya kuhusu mpango, kiwango na ukomo wa bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19.

Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Bunge, kinabainisha kuwa uwasilishwaji huo utafanywa leo na Waziri wa Fedha na Mipango, Philip Mpango katika mkutano wa wabunge wote. Mkutano wa wabunge wote kuhusu uwasilishwaji wa mapendekezo ya mpango, kiwango na ukomo wa bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19 utafunguliwa na kufungwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. Katika uwasilishaji huo, serikali itaainisha maeneo ya kipaumbele kulingana na mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka ujao wa fedha.

Baada ya kuwasilishwa, wabunge wanapewa nafasi ya kujadili kwa kina mapendekezo hayo, ikiwa ni kabla ya kuanza vikao vya Bunge la bajeti linalotarajia kuanza Aprili 3, mwaka huu. Bajeti ya serikali ya mwaka 2017/18 ilikuwa ni Sh trilioni 31.6 huku vipaumbele vikiwa ni pamoja na miradi ya makaa ya mawe Mchuchuma, chuma cha Liganga, ujenzi wa reli ya kati kutoka Dar es Salaam, Tabora hadi Kigoma yenye urefu wa km 1,251 kwa ‘standard gauge’ pamoja na matawi yake ya Tabora kupitia Isaka hadi Mwanza yenye urefu wa kilometa 379, Isaka hadi Rusumo kilometa 371, Kaliua kupitia Mpanda hadi Karema kilometa 321, Keza hadi Ruvubu kilometa 36 na Uvinza hadi Kelelema kuelekea Musongati yenye urefu wa kilometa 203.

Miradi mingine ilikuwa ni uboreshaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATC), ujenzi wa mitambo ya kusindika gesi mkoani Lindi, uanzishwaji wa Kanda Maalumu za Kiuchumi mkoani Tanga, Bagamoyo, Kigoma, Ruvuma, uanzishwaji wa kituo cha biashara cha Kurasini, kusomesha vijana katika stadi za mafuta na gesi, uhandisi na huduma za afya. Maeneo mengine ya kipaumbele yalikuwa ni viwanda vya kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa kukuza uchumi wa viwanda, kufungamanisha maendeleo ya uchumi na maendeleo ya watu, mazingira ya wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji, ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi pamoja na maeneo mengine muhimu kwa ukuaji wa uchumi na ustawi wa taifa.