Pilipili manga, mdalasini vyaingia soko la kimataifa

ZANZIBAR imetambulisha mazao manne ya pilipili manga, karafuu, mdalasini na pilipili hoho katika soko la kimataifa na kupata mwitikio kiasi ambacho bidhaa hizo zimekuwa chache.

Utambulisho huo uliofanywa mwishoni mwa mwaka jana ni bidhaa hizo zikiwa zimefungwa nzima nzima huku nyingine zikiwa zimetwangwa. Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC), Dk Said Seif Mzee alisema mchakato wa kuitambua karafuu na mazao mengine ulianza mwaka 2013, lakini kutokana na changamoto mbalimbali ilichukua muda mpaka mwaka jana.

Mzee alisema kutokana na soko la kimataifa kutaka bidhaa zinazoingia katika soko hilo kusajili wakulima wake, pia na Zanzibar imefanya hivyo licha ya kuwa bidhaa zake ni halisi. Aliweka wazi kuwa kwa kufuata taratibu tayari wakulima wa mazao hayo wamesajiliwa na kuthibitishwa na kampuni moja ya Kijerumani ambao wamehakikisha bidhaa hizo hazina kemikali ya aina yoyote.

Mkurugenzi huyo alisema bidhaa hizo zimependwa sana baada ya kupelekwa katika soko la kimataifa mwishoni mwa mwaka jana na kupata soko kubwa lakini bado bidhaa ni chache kutokana na kuwa kuna kipindi zinapotea kabisa. Alisema kwa kadri mazao yatakavyokuwa mengi licha ya kuongeza kipato cha mtu mmoja na serikali lakini itakuwa ikitangaza Zanzibar kimataifa.