Wanahabari washauriwa umuhimu wa Tehama, ubunifu

Mhariri Mtendaji wa Tanzania Standard Newspapers (TSN) Dkt Jim Yonazi ameshauri maofisa habari wa serikali kuwa wabunifu na kutoa habari kwa wakati ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia.

DK Yonaz ametoa ushauri huo leo wakati akitoa mada katika mkutano wa Maofisa Habari wa Serikali (TAGCO) jijini Arusha. “Ni vizuri mwanahabari wa zama hizi akawa nadhifu kimtizamo, kimuonekano na hata kiuwezo wa kujenga hoja anapohabarisha na huku ndiko kuongeza thamani kwa habari anazotoa” amesisitiza Dk Yonazi. Ameshauri matumizi ya Tehama katika kuhabari kwani kizazi cha sasa ndiko kilipo na akaongeza na kuongeza “inasaidia katika kasi ya kuhabarisha kwa haraka zaidi.”

Dkt Yonazi amewataka wanahabari wote kukubali kubadilika na kufuata mfumo ya teknolojia unavyotaka sasa huku akisisitiza “Ni vizuri kujenga uwezo mpya na mbinu mpya za kuhabarisha kwa kuwa wabunifu zaidi huku akitolea mfano kampuni anayoiongoza, TSN, ambayo kwa sasa imevuka mipaka ya nchi kupitia gazeti lake la HabariLeo ambalo hupatikana katika baadhi ya nchi za Afrika Mashariki, ikiwemo Rwanda.

Leo Jumanne, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari Maelezo, Dkt Hassan Abbas ameendesha mjadala wa pamoja huku akielezea vigezo anavyostahili kuwa navyo mwanahabari wa karne hii ya 21 ili kuivusha Tanzania kwenda uchumi wa kati. Akichangia mada hiyo, Katibu Mkuu wa TAGCO, Abdul Njahidi ambaye pia ni ofisa mawasiliano wa PSPF, ameipongeza sana TSN kwa kazi nzuri inayofanyika hivi sasa ya kuhabarisha kama chombo cha Serekali. Miongoni mwa wadhamini katika mkutano huo ni TSN, wachapati wa magazeti ya serikali; Daily News, Sunday News, HabariLeo, HabariLeo Jumapili na SpotiLeo.