Jiografia, amani Zanzibar mvuto kwa biashara

MAMLAKA ya Kukuza Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) imesema, jiografia ya Zanzibar, amani na maagizo ya Katiba ni kivutio kikubwa cha biashara na uwekezaji kuliko maeneo mengi Afrika hivyo watu waende wakazitumie fursa zilizopo.

Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Salum Khamis Nassor amesema jana ofisini kwake mjini Unguja kuwa, kwa kutambua hilo, visiwa hivyo vimepiga hatua kubwa katika kuvutia biashara na uwekezaji kwa kuwa karibu asilimia 60 ya huduma wanazohitaji wafanyabiashara na wawekezaji kwenye taasisi za serikali zinapatikana ZIPA.

Amesema, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inafanya juhudi kuondoa vikwazo vya kibiashara na uwekezaji vikiwemo vya upatikanaji vibali, usajili wa kampuni na ukaguzi wa maeneo ya ardhi kwa ajili wa kuwekeza.

“Biashara yoyote ni soko, na soko ni kulifuata, lipo soko litakufuata lakini kwa kiasi kikubwa soko ni kulifuata, jiographical location (ilipo Zanzibar kijiografia) ya Zanzibar katika Afrika, mahala ilipo, ni mahala peke yake ambapo mtu anaweza akafanya biashara na sehemu kubwa ya interior part (eneo la ndani) ya Afrika kwa urahisi zaidi…” amesema Nassor.

“Ni mahali ambapo meli ipo, Rwanda meli hakuna, kwa hiyo kama utataka kuchukua bidhaa kutoka mahali pengine popote duniani kufika Zanzibar ni rahisi kupitia kwenye Suez Canal, kwa hiyo utaikuta Zanzibar ipo almost at the Center of the world (katikait ya dunia)”amesema.

Nassor amesema, kwa namna Zanzibar ilipo, ni rahisi kufikika kwa namna tofauti na kwamba, visiwa hivyo vina faida kubwa kijiografia.

“…na kama ipo at the center of the world (katikati ya dunia) inafikika kwa njia yoyote ile tofauti na nchi nyingine, inafikika kwa ndege, inafikika kwa meli kwa hiyo ni rahisi kuja kufanya biashara hapa na nchi nyingine kutoka sehemu nyingine za dunia, globally (kidunia), Zanzibar imekuwa located mahala penye advantage (faida) kubwa globally” amesema.

Kwa mujibu wa Nassor, uimara wa siasa za Zanzibar na Tanzania kwa ujumla vina mvuto kibiashara kwa kuwa vinawahakikishia wafanyabiashara usalama.

“Biashara inahitaji mambo matatu makubwa, jambo la kwanza linahitaji security, na hii security huwezi kuipata kama nchi politically haipo stable, kwa hiyo stability ya politics za Zanzibar na Tanzania kwa ujumla zinasababisha sisi tuwe mahala peke yake ambapo mtu tunamshauri bora kuja hapa” amesema.

Amesema, serikali inahakikisha kwamba inalinda amani ili mazingira ya kufana kazi yanakuwa vizuri kwa ajili ya usalama wa watu na mali zao. Nassor amesema pia kuwa, Zanzibar imejiandaa vizuri kulinda mali ya mtu yeyote kwa mujibu wa ibara ya 17 ya Katiba ya nchi hiyo na ibarfa ya 17 ya Katiba ya Tanzania.

“Katiba inaagiza kwamba, mtu yeyote mwenye mali yake ndani ya nchi hii inapaswa ilindwe na ihifadhiwe, sawa, na isiweze kutumika kwa namna nyingine yoyote isiyokuwa kwa makubaliano na mwenyewe kwa maana ya kwamba, serikali pia serikali hairuhusiwi kugusa mali ya mtu mpaka mwenyewe awe tayari mali yake kutumika au kuwepo na sababu ambazo hazitaweza kuepukika lazima mali yake itumike na itakapotokea hiyo Katiba ndiyo inayoagiza kuwe na makubaliano ya kulipana fidia”amesema.

Nassor amesema, uwepo wa ZIPA umewezesha kurahisha shughuli za kibiashara na uwekezaji kwa kuwa kimekuwa ni kituo kimoja cha uwezeshaji biashara.

“Wakati unapotaka kumvutia mtu lazima kwanza uhakikishe unapendeza kwake, vinginevyo hutoweza kumvutia ikiwa hutokuwa unapendeza kwake kwa hiyo kumvutia mfanyabiashara, kumvutia mwekezaji lazima kufanya kwanza mazingira yetu yawe yanapendeza na kweli yanaweza yakamfanya aweze kufanya shughuli zake kwa urahisi na faida” amesema ofisini kwake.

Amezitaja baadhi ya mamlaka zilizopo kwenye jengo la ofisi za ZIPA kuwa ni ofisi ya kamishna wa kazi, uhamiaji, kamishna wa utalii, ofisi ya vibali vya ujenzi na ofisi ya msajili wa kampuni.

“Kwa hiyo mwekezaji anapokuja hapa katika siku chache au muda mfupi kadiri inavyowezekana anahakikisha anakamilisha taratibu zote za kisheria zinazotakiwa kwa ajili ya yeye kuweza kufanya shughuli zake hapa Zanzibar kwa kufuata sheria, tumejaribu kurahisha hivyo na imekuwa rahisi” amesema Nassor.