JPM aonya wanaokwaza wawekezaji wa viwanda

RAIS John Magufuli amewaonya watendaji wa wizara, mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri nchini kutokuwa kikwazo cha kukwamisha uwekezaji wa viwanda katika maeneo yao na kutaka wawe mstari wa mbele kutoa msaada pale inapohitajika.

Pia amewataka viongozi waliopewa madaraka kuanzia ngazi za Waziri Wakuu, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi watendaji, maofisa tarafa na wengineo wawe ni watatuzi wa kero za wananchi wanyonge na si kuwa sehemu ya kutengeneza kero. Rais Magufuli alisema hayo wakati akiwahutubia mamia ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya mji wa Morogoro baada ya kuzindua kiwanda kipya cha kutengeneza sigara aina ya Marlboro cha Philip Morris Tanzania Limited (PMT) kilichopo Mkambarani, Wilaya ya Morogoro.

Alisema kila kiongozi wa serikali katika sehemu alipo anapaswa kushughulikia kero za wananchi wanyonge badala ya kuwa ni chanzo cha kero hizo kwa kuwa si kila kero inapaswa itatuliwe na Rais. Rais Magufuli alisema kuwa vipo vitu vidogo vidogo vinaweza kutatuliwa na watendaji wa ngazi za chini, lakini hazitatuliwi na kufanya wananchi waendelee kulalamikia nahata kuzifikisha malalamiko yao kwa Rais.

Moja ya kero ambazo wanapaswa kusimamia na kuziondoa ni kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara kwa wafanyabiashara wadogo, wakiwemo mamalishe kwa kutowabughudhi kwenye maeneo yao ya kufanyia biashara. Kuhusu uwekezaji wa viwanda, Rais Magufuli alisema kiwanda hicho cha kutengenza sigara kitasaidia kuondoa kero ya wakulima wa zao la tumbaku hasa wa mikoa inayozalisha zao hilo, ukiwemo wa Tabora.

Rais alisema kiwanda hicho cha tatu cha kutengeneza sigara nchini pia kitasaidia upatikanaji wa soko la uhakika na wakulima kupata bei nzuri na kuongeza ajira kwa vijana na mapato ya serikali kupitia ulipaji kodi. Alisema serikali yake anayoiongoza itahakikisha inaendelea kuweka mazingira mazuri ya kuboresha uwekezaji wa viwanda chini ili wananchi waweze kufaidi matunda ya uhuru wao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Shanif Mansoor Hiran alisema kampuni hiyo ilisajiliwa Oktoba 16, mwaka 2015 na kuanza kujenga kiwanda cha kuzalisha na kuuza bidhaa za tumbaku na hasa sigara aina ya Marlboro mkoani Morogoro. Alisema kwa sasa kiwanda hicho kitaanza kwa kuzalisha sigara milioni 400 kwa mwaka na kitachangia kulipa mapato ya Sh bilioni 12 kwa serikali na kutoa ajira za awali kwa Watanzania 224.

Alisema kuwa kiwanda hicho ni kikubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki ambacho kimejengwa eneo la Mkambarani katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro. Naye Mwekezaji katika kiwanda hicho kutoka kampuni tanzu ya Philip Morris International (PMI), Dagmar Piaseck alisema uwekezaji umegharimu Sh bilioni 65 za kitanzania. Alisema kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kutengeneza aina ya sigara za Marlboro bilioni moja katika awamu ya kwanza na katika awamu ya pili bilioni 0.5. Alisema ujenzi wa kiwanda hicho ni moja ya juhudi za kuiunga mkono serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Magufuli na kwamba sigara zitakazotengenezwa zitakuwa na ubora wa kimataifa.