TSN kukutanisha mawaziri pande zote za muungano

KAMPUNI ya Magazeti ya Serikali (TSN) kupitia Jukwaa la Fursa za Biashara leo inawakutanisha mawaziri kutoka pande mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kusaka fursa za biashara katika visiwa vya Zanzibar.

Jukwaa hilo litafanyika katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi katika Mkoa wa Mjini Magharibi. Mbali na mawaziri hao, wadau mbalimbali wakiwemo Mwenyekiti wa Bodi ya TSN, Hab Mkwizu wanatarajiwa kuhudhuria jukwaa hilo litakalokuwa na wajumbe zaidi ya 350 wakiwemo kutoka kampuni kubwa 50 kufichua fursa zilizopo lakini bado hazijafanyiwa kazi.

Miongoni kwa mawaziri watakaohudhuria ni pamoja na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk HarrisonMwakyembe na Waziri wa Viwanda na Biashara, Balozi Amina Salum Ali, Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mahamoud Thabit Kombo na wengineo. Meneja Mauzo na Masoko wa TSN, Januarius Maganga alisema Jukwaa la Fursa za Biashara Zanzibar litawezesha kufahamika kwa fursa zaidi visiwani humo kwa kuwa si zote zinazofahamika.

Maganga alisema jukwaa hilo limeandaliwa kwa ushirikiano wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, na Baraza la Biashara Zanzibar. Kwa mujibu wa Maganga, jukwaa hilo linalotarajiwa kuwa na wajumbe zaidi ya 350 wakiwemo kutoka kampuni kubwa 50 litakuwa na washiriki wa aina tatu wakiwemo wadhamini, wadau, watakaoalikwa na kamati ya maandalizi na wawakilishi wa TSN.

Jukwaa hilo limedhaminiwa na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Benki ya Azania, Benki ya NMB, Benki ya Watu wa Zanzibar (ZPB), Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji Zanzibar (ZURA), Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA).

Wengine ni Nabaki Afrika, Kampuni ya VIGOR Group, Hoteli za The Dream,The Africa House Hotel, Park Hyatt Hotel, Mfuko wa Barabara Zanzibar, Shirika la Umeme Tanzani (TANESCO), Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji Tanzania (EWURA) Bohari ya Dawa (MSD), Watumishi Housing, Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (Neec) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Majukwaa ya biashara yanayoandaliwa na Kampuni ya TSN inayochapisha magazeti ya Daily News, HabariLeo na SpotiLeo yalianza Februari mwaka jana mkoani Simiyu, yameshafanyika mengine manne katika mikoa ya Mwanza,Tanga, Shinyanga na jukwaa hilo la tano likiwa la kwanza mwaka huu.