Kampuni ya magazeti TSN kubadilishwa

MHARIRI Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Dk. Jim Yonazi amesema, muda si mrefu kampuni hiyo itabadilika na itajulikana kwa jina la TSN Media Services Group.

Dk Yonazi ameyasema hayo kwenye ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi mjini Unguja wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Fursa za Biashara Zanzibar.

Jukwaa hilo ni la kwanza la TSN kufanyika Zanzibar ila ni la tano tangu kampuni hiyo ianze kuandaa majukwaa ya fursa za biashara. majukwaa kama hayo tayari yamefanyika kwenye mikoa ya Simiyu, Mwanza, Tanga na Shinyanga.

Jukwaa hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Zanzibar na Tanzania bara akiwemo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, na Mwenyekiti wa Bodi ya TSN, Hab Mkwizu.

Dk. Yonazi amesema, TSN imejidhatiti kutoa huduma za habari na kwamba, kwa sasa kampuni hiyo licha ya kuchapisha magazeti, inatengeneza vipindi vya televisheni ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) vinavyorushwa na chaneli ya TB1 ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Pia amewaeleza wajumbe wa jukwaa hilo wakiwemo mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuwa, TSN pia inachapisha machapisho mbalimbali vikiwemo vipeperushi, inatengeneza matangazo ya biashara na mabango.

Amesema, wamekubaliana na viongozi wa Zanzibar ushirikiano wa TSN na visiwa hivyo uwe wa kudumu, na kwamba, kampuni hiyo inajisikia fahari kuona fursa zinaanza kuleta mabadiliko.

Dk. Yonazi amesema, TSN inaandaa majukwaa hayo kuibua fursa za kiuchumi na maendeleo katika nchi yetu.

Kwa mujibu wa kiogozi huyo, kampuni hiyo imedhamiria kuendelea kutoa habari zenyer thamani zinazomuwezesha mtu kufanya uamuzi ili zilete tofauti katika maisha ya watu.

Amesema, TSN itaendelea kuandaa majukwaa ya fursa za biashara na kwamba, litakalofuata litafanyika Arusha.