TSN yafanikiwa kutangaza fursa za Zanzibar

MHARIRI Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Dk. Jim Yonazi amesema, kampuni hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuzitangaza fursa zilizopo Zanzibar.

Dk. Yonazi amesema, TSN itaendelea kuandaa majukwaa ya fursa za biashara, na kwamba, ina uzoefu wa kutosha wa takribani miaka 88 unaoiwezesha kuwatumikia Watanzania.

Dk Yonazi ameyasema hayo kwenye ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi mjini Unguja wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Fursa za Biashara Zanzibar.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa TSN, kampuni hiyo itaandaa majukwaa ya kisekta zikiwemo za madini, nishati, utalii na nyinginezo.

Amesema, imejipanga, na kwamba, itafanya majukwaa hata nje ya nchi kwa mfano, Dubai, Oman na kwingineko.

Jukwaa la Zanzibar limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Zanzibar na Tanzania bara akiwemo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, na Mwenyekiti wa Bodi ya TSN, Hab Mkwizu.

Dk. Yonazi amesema, TSN imejidhatiti pia kutoa huduma za habari , na kwamba, kwa sasa kampuni hiyo licha ya kuchapisha magazeti ya serikali, inatengeneza vipindi vya televisheni ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) vinavyorushwa TB1.

Dk. Yonazi pia amewaeleza wajumbe wa jukwaa hilo wakiwemo mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuwa, TSN pia inachapisha machapisho mbalimbali vikiwemo vipeperushi, inatengeneza matangazo ya biashara na mabango.

Amesema, wamekubaliana na viongozi wa Zanzibar ushirikiano wa TSN na visiwa hivyo uwe wa kudumu, na kwamba, kampuni hiyo inajisikia fahari kuona fursa zinaanza kuleta mabadiliko.

Dk. Yonazi amesema, TSN inaandaa majukwaa hayo kuibua fursa za kiuchumi na maendeleo katika nchi yetu.

Kwa mujibu wa kiogozi huyo, kampuni hiyo imedhamiria kuendelea kutoa habari zenye thamani zinazomuwezesha mtu kufanya uamuzi ili zilete tofauti katika maisha ya watu.