‘Mahitaji majukwaa ya fursa ni makubwa’

MWENYEKITI wa Bodi ya Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Hab Mkwizu amesema, kuna mwitikio mkubwa katika majukwaa ya fursa za biashara na mahitaji yanaongezeka.

Mkwizu amesema, jukwaa linalofanyika leo Zanzibar ni moja ya kazi za ubunifu za kampuni hiyo na kwamba TSN inatekeleza jukumu lake la kuchangia maendeleo ya taifa.

Ameyasema hayo leo kwenye mkumbi wa Baraza la Wawakilishi mjini Unguja wakati wa ufunguzi wa jukwaa la fursa za biashara Zanzibar.

“Kwa sasa tuna maombi ya kuendesha majukwaa haya karibu mikoa yote, na sisi TSN tumejipanga kwenda kote huko” amesema Mkwizu.

Alisema, jukwaa la Zanzibar lina lengo la kuibua fursa za maendeleo ya kiuchumi kwa ajili ya wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

“Huu ni mwendelezo na sio mwisho wa juhudi za TSN kusukuma maendeleo ya Zanzibar. Tutaendelea kushirikiana na mamlaka mbalimbali katika kuendelea kusaidia maendeleo kwa kuibua fursa katika sekta mbalimbali” amesema Mkwizu.

Awali, Mhariri TSN, Dk. Jim Yonazi alisema, kampuni hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuzitangaza fursa zilizopo Zanzibar.

Dk. Yonazi amesema, TSN itaendelea kuandaa majukwaa ya fursa za biashara na kwamba, ina uzoefu wa kutosha wa takribani miaka 88 unaoiwezesha kuwatumikia Watanzania.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa TSN baada ya jukwaa la Zanzibar kampuni hiyo itaandaa majukwaa ya kisekta zikiwemo za madini, nishati, utalii na nyinginezo.

Amesema, imejipanga na kwamba, itafanya majukwaa hata nje ya nchi kwa mfano, Dubai, Oman na kwingineko.

Jukwaa la Zanzibar limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Zanzibar na Tanzania bara akiwemo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, na Mwenyekiti wa Bodi ya TSN, Hab Mkwizu.

Amesema, wamekubaliana na viongozi wa Zanzibar ushirikiano wa TSN na visiwa hivyo uwe wa kudumu, na kwamba, kampuni hiyo inajisikia fahari kuona fursa zinaanza kuleta mabadiliko.

Dk. Yonazi amesema, kampuni hiyo imedhamiria kuendelea kutoa habari zenye thamani zinazomuwezesha mtu kufanya uamuzi ili zilete tofauti katika maisha ya watu.