Fursa za biashara Zanzibar hizi hapa

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd amesema ili kufufua na kujenga viwanda katika visiwa hivyo vitakavyofanya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ifanikiwe azma ya kufi kia uchumi wa kati, lazima fursa nyingi zitapatikane na kutumia malighafi za nchini kwa gharama nafuu.

Alisema fursa nyingi zitapatikana kwani viwanda vingi vinahitaji mazao yatokanayo na kilimo, mifugo na rasilimali nyingine zilizoko baharini na ardhini kama vile mafuta, gesi na madini ya aina mbalimbali. Alisema hayo jana mjini hapa wakati akifungua Jukwaa la Fursa za Biashara Zanzibar lililoandaliwa na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), wachapishaji wa magazeti ya HabariLeo, HabariLeo Jumapili, HabariLeo Afrika Mashariki, Daily News, Sunday News na SpotiLeo litakalovutia zaidi wawekezaji.

Katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa nchi, ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif alisema jukwaa hilo litahamasisha uwekezaji wa viwanda vidogo na vya kati ili kuongeza uzalishaji na tija na kutoa fursa za ajira kwa wananchi hasa vijana na akinamama na hivyo kuongeza kipato na kuinua uchumi wa Zanzibar kwa jumla.

Jukwaa hilo lilihudhuriwa pia na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, Waziri wa Viwanda Biashara na Masoko Zanzibar, Balozi Amina Salum Alli, Waziri wa Habari, Utamaduni na Mambo ya Kale Zanzibar, Mahamoud Thabit Kombo na wadau wengine na wajumbe zaidi ya 350 wakiwemo kutoka kampuni kubwa 50, mabalozi wadogo kutoka India, China na Oman. Balozi Seif alisema kwa kutumia jukwaa hilo, zitapatikana fursa za kubadilishana taarifa kwa wazalishaji au watoaji malighafi na watumiaji wa malighafi hizo.

Alisema Zanzibar ni visiwa vyenye utajiri pekee wa maliasili ambazo zitatumika kikamilifu zinaweza kubadilisha maendeleo ya watu wake na Tanzania. “Sekta ya utalii, ina vivutio vyenye sifa lukuki. Kwa bahati mbaya vivutio hivyo havifahamiki na pia hamasa kuvitangaza, kuviendeleza na kufanya uwekezaji iko chini,” alisema. Alisema hiyo inaonesha kuna uhitaji mkubwa wa kuweka mkazo kujitangaza na kuendeleza na kutumia rasilimali zilizowazunguka.

Balozi Iddi alisema visiwa vya Zanzibar na pemba vimezungukwa na bahari na hivyo kuwa sehemu yenye rasilimali nyingi za bahari ikiwemo wingi wa samaki, dagaa, mwani, chumvi na mazao na kuwa fursa zipo katika kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani na kusarifu mazao hayo.

Alisema Zanzibar pia ni maarufu kwa mazao ya viungo ikiwemo Karafuu, hiliki, Mdarasini, Pilipili Manga na vinginevyo hivyo kuna fursa za kuwekeza katika kuongeza uzalishaji na kuanzisha viwanda vya kusanifu na kuongeza thamani katika mazao hayo kwa kutengeneza mafuta, hiliki na dawa ili kulifikia soko la ndani na masoko ya kimataifa kwa bidhaa zenye viwango vya ubora na vilivyoongezwa thamani.

Akizungumza jukwaa hilo, alisema lengo lake ni kuchangamsha uchumi wa Zanzibar kwa kuwakutanisha wahusika wa maendeleo ya kiuchumi ili wafahamiane kujenga uhusiano kuleta maendeleo ya uchumi. “Kwa kutumia jukwaa hili, Zanzibar itapata fursa ya kujitathmini kupitia aina nyingine ya mtazamo wa kibiashara tofauti na uliozoeleka. Fursa mbalimbali zinabainishwa kwa washiriki kueleza mapya mazuri waliyonayo na ya zamani yaliyoboreshwa kukidhi mazingira ya sasa ya maendeleo ya visiwa hivyo,” alisema.

Alisema wananchi wa visiwa hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kutatua changamoto zilizopo kisha kuchuma matunda ya fursa hizo zinazowazunguka na kuwataka kuondokana na dhana ya kusubiri watu wengine wafikirie kwa ajili yao kwani hawatawaza kwa faida yao kwa asilimia 100 bali watabakiza pa kuwabana ili kuendelea kuwa tegemezi hivyo ni vema kukataa mazingira hayo.