TSN mbioni kubadili jina

KAMPUNI ya Magazeti ya Serikali (TSN) wachapishaji wa magazeti ya HabariLeo, HabariLeo Jumapili, Habarileo Afrika Mashariki, Dailynews, Sunday News na Spoti Leo hivi karibuni inatarajia kubadili jina kuwa TSN Media Services Group.

Hatua ya kubadilisha jina inatokana na namna kampuni hiyo inavyobadilisha utoaji huduma zake kutoka kuchapisha magazeti ya serikali pekee na sasa kutoa huduma mbalimbali za masuala ya habari nchini.

Mhariri Mtendaji wa TSN, Dk Jim Yonazi alisema hayo jana wakati akiwakaribisha wadau mbalimbali wa Jukwaa la Fursa za biashara Zanzibar lililoandaliwa na TSN kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais Zanzibar, Baraza la Biashara Zanzibar pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi.

Alisema kampuni hiyo imejidhatiti kutoa huduma za habari kwa kuandaa vipindi ikishirikiana na wadau vikiwemo vya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) vinavyorushwa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC). Mbali na kuandaa vipindi, TSN pia wanatoa huduma za uchapaji, kutengeneza matangazo ya aina mbalimbali, mabango, vipeperushi na mengineyo.

Kwa muda sasa imeendelea kukua kibiashara. Dk Yonazi alisema majukwaa mbalimbali ambayo TSN imekuwa ikiandaa yamelenga kuibua fursa za uchumi na maendeleo kwa kuelimisha wananchi habari zenye thamani na kuwawezesha kufanya maamuzi. Mwenyekiti wa Bodi ya TSN, Hab Mkwizu alisema mpango huo ulibuniwa mwaka jana na TSN kuibua fursa za uchumi katika mikoa na kuhamasisha wananchi wa maeneo hayo kuzitumia kujiletea maendeleo.