Samia awezesha Bil 1.7/- za ujenzi hospitali ya Muheza

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewezesha kupatikana kwa Sh bilioni 1.7 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Muheza mkoani Tanga.

Katika hafla ya kuchangia ujenzi huo uliofanyika kwenye Hoteli ya Golden Tulip jijini Dar es Salaam juzi, Makamu wa Rais aliupongeza uongozi wa Wilaya ya Muheza na Mkoa wa Tanga pamoja na wananchi kwa kuamua kujenga hospitali yao ya wilaya ili kuboresha hali ya afya na ustawi wa jamii. Makamu wa Rais alisema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuimarisha ubora wa huduma za afya ikiwa ni pamoja na kupunguza idadi ya vifo vya watoto kutoka kiwango cha vifo 66 kati ya vizazi hai 1,000 hadi kufikia kiwango cha angalau vifo 40 kati ya vizazi hai 1,000.

Aidha, alisema serikali imedhamiria kupunguza vifo vya wanawake wajawazito kutoka 556 kwa mwaka 2017 katika vizazi hai 100,000 hadi kufikia 292 ifikapo mwaka 2020. “Sambamba na hilo, serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo tuna mkakati wa kujenga, kukarabati na kupanua miundombinu ya vituo vya afya 208 ili kuimarisha utolewaji wa huduma mbalimbali za afya,” alisema.

Makamu wa Rais ameutaka uongozi wa Mkoa wa Tanga na wa Wilaya ya Muheza kuupa kipaumbele mradi huo wa ujenzi wa hospitali ya wilaya na kuhakikisha wanaweka mradi huu katika bajeti zinazokuja pamoja na kutafuta wahisani wengine wa ndani na nje ya nchi ili kuwezesha ujenzi wa hospitali hiyo kukamilika kwa haraka. Makamu wa Rais aliwashukuru wadau wote walioshiriki na kuomba kila mmoja achangie kwa uwezo na nafasi yake ili hospitali ya Wilaya ya Muheza ikamilike mapema.

Mbunge wa Jimbo la Muheza, Balozi Adadi Rajab alimshukuru Makamu wa Rais kwa kuwezesha kufanikisha kupatikana kwa mchango mkubwa ambao hawakuutegemea. Aliahidi ili kuuenzi mchango huu na mapenzi ya Makamu wa Rais, kwa wanaMuheza basi watahakikisha hospitali hiyo au jengo lolote lile la hospitali hiyo linapewa jina la Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo pamoja na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu. Hivi sasa Wilaya ya Muheza iliyoanzishwa mwaka 1974, haina Hospitali ya Wilaya na wananchi wanaohitaji huduma za afya wamekuwa wakitumia Hospitali Teule (DDH) ya Kanisa la Anglikana ambayo imeingia mkataba na serikali na kutokana na idadi ya wananchi wa wilayani hapo, hospitali hiyo imezidiwa.

Mkuu wa wilaya hiyo, Mwanasha Tumbo, tayari wananchi na wadau wa maendeleo Muheza na Watanzania kwa ujumla wameanza kuchangia ujenzi huo na hadi kukamilika kwake zinahitajika Sh bilioni 11.1, hivyo wakati wakisubiri fedha za Serikali Kuu na zile za kwenye bajeti, wameamua kuanza kwa kuchangisha fedha hizo.