Masasi warejesha shuleni waliokatishwa kwa mimba

CHUO cha Maendeleo ya Wananchi wilayani Masasi mkoani Mtwara, kimeanza kusajili wanafunzi wa shule za msingi na sekondari waliokatishwa masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo ndoa za utotoni pamoja na waliopata ujauzito ili vijana hao waendelezwe kielimu hatimaye watimize ndoto zao za maisha.

Hayo yamesemwa hapa na Mkuu wa chuo hicho, Fred Mwakagenda akizungumza na gazeti hili ofisini kwake kuhusu maendeleo ya chuo hicho na changamoto zilizopo na namna uongozi ulivyojipanga kukiendeleza.Mwakagenda alisema chuo hicho kupitia mpango maalumu kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Karibu Tanzania Organization (KTO) na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeazimia kutekeleza mpango maalumu kwa kuzingita mpango wa serikali wa elimu jumuishi.

Alisema mpango huo wa kutaka kuchukua wanafunzi waliokatishwa masomo kwa sababu mbalimbali na kujikuta wakiwa nyumbani huku baadhi yao wakitamani kuendelea na masomo, unalenga kutoa fursa ya kupata elimu ya mafunzo ya ufundi, stadi za maisha, stadi za fedha na ujasiriamali kwa kuchanganya na masomo ya sekondari. Alisema wanafunzi hao watapatiwa elimu hiyo katika mfumo usio rasmi kwa kupitia Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima na kwa kutumia vyuo maendeleo ya wananchi kama vituo vya kutoa elimu hiyo na kufanyia mitihani.

Mwakagenda alisema mpango huo ni njia mbadala ya kuwasaidia wanawake na vijana kusonga mbele kwenye maisha na kuchangia kwenye kuinua uchumi wa Taifa, kwa wanawake vijana waliokatishwa masomo shuleni kwa sababu mbalimbali ikiwemo ndoa za utotoni, kukimbia ukeketaji pamoja na kupata ujauzito.

Alisema vyuo vifuatavyo vimo katika programu ya majaribio kati ya vyuo 20 vitakavyoendesha programu hiyo kabambe; ambavyo ni Mbinga FDC, Masasi FDC, Bigwa FDC na kwamba umri wa vijana ambao wanahitajika kufanyiwa usajili ni umri usiozidi miaka 25 Alisema wanawake na vijana wengine ambao pia watachukuliwa kuwapo katika programu hiyo ni wale wenye umri wa miaka 17 hadi kufikia 30, na kwa kijana mwenye mtoto atapaswa kulipa ada ya Sh 250,000 kwa kukaa bweni kwa mwaka na mwanamke kijana mwenye mtoto anayechagua kozi ya kutwa atalipa ada ya Sh 150,000. Aliongeza kuwa wanawake vijana wengine wakiwamo wanavikundi vya benki za kijamii vijijini (Vicoba), watalipa ada ya Sh 450,000 kwa mwaka kwa watakaokaa bweni.