Chai maharage, makubazi ‘ladha’ Zanzibar

MHARIRI Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Dk Jim Yonazi ametaka wananchi wa Zanzibar kutumia magari ya ‘chai maharage’ kubeba watalii kutoka uwanja wa ndege na kuwapeleka sehemu nyingine.

Alisema magari hayo ya kipekee yanayotumika zaidi Zanzibar pamoja na viatu vya makubazi vitumike katika utalii kutokana na upekee wake ili kuongeza fursa. Dk Yonazi alisema pia chakula cha urojo nacho kinaweza kutumika kama fursa ya kutangaza kwa watalii kutokana na upekee wake Zanzibar. Aliahidi kufanya majukwaa zaidi ya biashara nchini ikiwemo ya kulinda nguvukazi ya vijana katika kupambana na dawa za kulevya.

Aidha, alisema pia kutakuwa na majukwaa ya wajasiriamali na yale ya kisekta baada ya kuona mafanikio makubwa katika majukwaa ya fursa ya biashara yaliyokwishafanyika. Dk Yonazi alisema hayo wakati akihitimisha Jukwaa la Fursa za biashara Zanzibar lililofanyika Ijumaa na kufanyika kwa mafanikio makubwa kutokana na kujitokeza kwa watu wa kada mbalimbali. Miongoni mwa waliohudhuria tamasha hilo, mbali na Mawaziri na wakuu wa taasisi mbalimbali vijana kutoka pande zote za visiwa hivyo.